SIMANJIRO-MANYARA
Katika Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara asilimia 80 ni wafugaji na ufugaji ndiyo kazi kubwa inayowapatia kipato na chakula, kutokana na hali hiyo Wananchi wa vijiji 6;wamepatiwa elimu ya kukabiliana na matukio yatokanayo na mabadiliko ya hali ya hewa katika sekta za mifugo, kilimo, uvuvi, na uchimbaji wa madini.
Akizungumza katika kijiji cha Korongo wilayani humo Afisa ufuatiliaji na Tathmini wa Mradi wa Ardhi Yetu kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Jumuiko la MaliAsili Tanzania (TNRF) Bwana Rogath Massay amesema kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania wanaijengea jamii uwezo kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kuondoa changamoto mbalimbali ikiwemo ya taarifa kutofika kwa wakati kwa wananchi.
Wananchi walioshiriki mafunzo hayo ya siku mbili wamelishukuru Shirika la Jumuiko la MaliAsili Tanzania (TNRF) kuona umuhimu wa kuwapatia mafunzo juu ya kupata taarifa za tabiri za kiasili na Kisayansi; huku wakitoa wito kwa wadau kuendelea kushirikiana na serikali kuwajengea uwezo zaidi ili waweze kukabiliana na majanga katika maeneo yao.
Aidha wsahiriki hao wameelezea viashiria vya kiasili vinavyotumika kutoa taarifa za utabiri wa kiasili kwa wananchi huku wakieleza vikwazo vilivyowafanya wasifikie malengo msimu wa vuli uliopita baada ya kupatiwa mafunzo hayo.
Afisa Kilimo Wilaya ya Simanjiro Bi Jenifa Mbuya amesema taarifa za tabiri za hali ya hewa za kijadi na kisayansi ni msaada mkubwa kwa wakulima na wafugaji ingawa baadhi ya taarifa zinakosekana kutokana na wazee wa zamani waliokuwa wakitabiri wengi wao kufariki dunia, na kuwataka wazee wa sasa kuweka kumbukumbu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Daktari wa Mifugo Wilaya ya Simanjiro Yasini Mshana amesema taarifa za tabiri za kijadi na kisayansi ni muhimu kwa shughuli za kila siku za ufugaji kwani zinatoa mwanga kwa wafugaji kujua ni wapi wawekeze nguvu zao kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Mazingira Wilaya ya Simanjiro Bwana Jovin Rweyemamu amesema zamani utabiri wa kijadi ulikuwa na nguvu tofauti na sasa; wananchi wanategemea zaidi utabiri wa kisayansi kutokana na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi yanayosababishwaa na uharibifu wa mazingira.
Aidha Mtabiri wa Hali ya Hewa kitengo cha utafiti, mazingira, na Matumizi Ya Hali Ya Hewa Bibie Abdallah amesema lengo kubwa la mafunzo hayo ni kutoa uelewa kwa wakulima na wafugaji juu ya taarifa za hali ya hewa ili kuwasaidia katika shughuli zao za kila siku za kilimo na ufugaji.
Vijiji vilivyonufaika kwa mafunzo hayo kupitia mradi wa Ardhi yetu unaosimamiwa na Shirika la Jumuiko la MaliAsili Tanzania (TNRF) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ni Korongo, Magadini, Kitwai A na B, Olchoronyori, pamoja na Loonderkes vilivyopo Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇