Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro Mathayo Masele
wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Halmashauri ya wilaya ya
Malinyi unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) akiwa katika
ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi mkoani Morogoro
mwishoni mwa wiki. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
(Kulia) akielekea kukagua ofisi za Ardhi za halmashauri ya wilaya ya
Ulanga wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi
mkoani Morogoro mwishoni mwa wiki. Wa pili kulia ni Mkuu wa wilaya ya
Ulanga Ngollo Malenya na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Ulanga Juma Kapilima.
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimpa
maelekezo Mkuu wa Idara ya Ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Ulanga
Luis Ndumbaro wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya
ardhi mkoani Morogoro mwishoni mwa wiki. Kulia kwa Naibu Waziri ni Mkuu
wa wilaya ya Ulanga Ngollo Malenya.
****************************
Na Munir Shemweta, WANMM ULANGA
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula
amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro
kumpatia maelezo kuhusiana na uamuzi wake wa kuondoa kasma ya ardhi na
mipango miji kwenye bajeti ya mapato ya ndani baada ya sekta hiyo
kuhamishiwa Wizarani.
Uamuzi
huo wa Dkt Mabula unafuatia kuelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Ngollo
Malenya kuwa moja ya changamoto inayoikabili sekta ya ardhi kwenye
wilaya yake ni ukosefu wa fedha za uendeshaji wa ofisi uliosababishwa na
halmashauri kuondoa kasma ya ardhi na mipangomiji baada ya sekta hiyo
kuhamia wizara ya ardhi jambo alilolieleza limesababisha utekelezaji
majukumu ya kila siku kuwa magumu.
Akiwa
katika ziara yake ya siku moja katika wilaya hiyo mwishoni mwa wiki,
Naibu Waziri huyo wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alimtaka Kaimu
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ulanga Juma Kapilima kumpa
taarifa ya maandishi kuhusiana na suala hilo kwa kuwa Waraka uliotolewa
kuhusiana na suala hilo unaeleza wazi kilichohamishiwa wizarani ni
Mamlaka ya Nidhamu na Ajira pekee.
‘’Hii
ni serikali moja, ofisi ya Mkurugenzi ni Mamlaka ya upangaji, nataka
maelezo ya msingi maana waraka unajieleza na ulienda kwa Makatibu Tawala
wa Mikoa na Wilaya na hata mishahara ya watumishi wa sekta ya ardhi
bado inalipwa na TAMISEMI’’ alisema Dkt Mabula,
Kwa
mujibu wa Mkuu wa wilaya ya Ulanga, mbali na changamoto ya ukosefu wa
fedha katika sekta ya ardhi, wilaya yake inakabiliwa pia na uchache wa
watumishi hususan katika fani za Mipango Miji, Uthamini, Uchoraji Ramani
na Watunza Kumbukumbu alioueleza kuwa unasababisha shughuli
zilizopangwa kutofanyika kwa ufanisi.
Aidha.
Naibu Waziri Mabula alionesha kutoridhishwa na kasi ya zoezi la
urasimishaji na upimaji viwanja kwenye wilaya ya Ulanga na kueleza kuwa
halmashauri hiyo inatakiwa kuongeza kasi katika mazoezi hayo mawili ili
kuwa na mji uliopangika na kuepuka ujenzi holela.
Aliongeza
kwa kusema, katika zoezi la urasimishaji linaloendelea nchini
halmashauri ya Ulanga inatakiwa kukaa na wananchi pamoja na makapuni ya
urasimishaji ili kukubaliana gharama za urasimishaji na kusisitiza
kiwango cha shilingi 150,000 kilichowekwa na Wizara kinaweza kupungua
ili kuwafanya wananchi wengi kushiriki,
‘’Kuna
halmashauri zimekubaliana na makampuni ya urasimishaji ambapo gharama
zimepungua hadi kufikia 60,000 hivyo ninyi hapa msing’ang’anie kiwango
cha 150,000 maana kinaweza kupungua kulingana na ugumu wa kazi na idadi
ya watu waliojitokeza kurasimishwa’’. Alisema Dkt Mabula
Katika
hatua nyingine Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt
Angeline Mabula ametembelea wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro na kuitaka
wilaya hiyo kuongeza kasi ya upimaji, upangaji na umilikishaji ardhi na
kuzingatia kupanga mji wa kiserikali utakaojumuisha taasisi zote za
umma.
Aidha,
Dkt Mabula alikagua ujenzi wa jengo la halmashauri ya wilaya ya Malinyi
pamoja na nyumba ya Mkuu wa wilaya unaofanywa na Shirika la Nyumba la
Taifa (NHC) ambapo alionesha kufurahishwa na kasi ya ujenzi wa majengo
hayo mawili yanayotarajiwa kukabidhiwa rasmi mwanzoni mwa mwaka ujao
2020.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇