LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Nov 27, 2019

KATIBU MKUU WA CCM DK.BASHIRU ASHIRIKI HAFLA YA MAULID, KISIWANI TUMBATU, ZANZIBAR

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. Bashiru Ally Kakurwa, amesema viongozi na waumini wa dini mbali mbali wana mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi.

Amesema hayokatika hafla ya Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad  (S.A.W) iliyofanyika kwenye Msikiti wa Gomani katika Kisiwani Tumbatu, Zanzibar, jana.

Katika Maulid hayo ambayo ni makubwa katika Kisiwa hicho yaliyofanyika Novemba 26,  2019  sawa na mwezi 28 mfungo sita 1441 Hijjiria Dk. Bashiru alieleza kuwa japokuwa Serikali haina dini lakini inatambua mchango wa dini mbalimbali katika maendeleo ya nchi, na kwamba mchango mkubwa wa taasisi hizo za kiimani katika maendeleo unaotakiwa kulindwa na kuenziwa kwa gharama yoyote.

Alisema kinachozuiwa ni tabia za kuendekeza imani kali za kidini zinazosababisha madhara ya kuchonganisha, kubaguana na kufarakanisha jamii na kusababisha machafuko na migogoro ya kuharibu Amani ya nchi.

"Miiko ya muumini yeyote ndio miiko ya raia mwema yoyote, masharti ya dini yoyote ndio masharti ya Serikali yoyote yenye ustawi wa maendeleo. Tuna kila sababu ya kulinda tunu hii ya amani na utulivu wa nchi ambayo msingi wake ni uwezo wa uhuru wa kuabudu bila mipaka, na kila Mwananchi kuheshimu dini ya mwenzake.'' alisema Dk. Bashiru.

Aliwakumbusha waumini wa dini hiyo kila wanapokutana wakumbushane historia ya uhuru wa dini uliopo hivi sasa nchini na kuongeza kuwa amani na utulivu wa nchi havikupatikana hivi hivi bali bali umetokana na juhudi za Serikali zote mbili ya Tanzania Bara na Zanzibar, zilizofanya kazi ya ziada ya uwepo wa misingi hiyo.

Alisema viongozi wa dini wanaoelekea katika uzeeni na wale waliofariki wanatakiwa kila Maulid kukumbukwa mchango wao walioutoa katika huduma za kiimani kwani wao ni alama tosha ya kupanda mbegu bora ya kiimani kwa watoto na vijana wa kiislamu.

Katibu Mkuu huyo akitoa nasaha zake, alisema daima waumini wa dini hiyo wathamini na kuenzi juhudi za waasisi Taifa ambao ni Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Karume na Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwani ndio waliopigania uwepo wa haki ya uhuru wa kuabudu.

Katika maelezo yake Dk.Bashiru, aliwataka Vijana wa Tumbatu kulinda Historia iliyotukuka ya Maulid hayo ya kiimani na kijamii ili yaendelee kufanyika kwa ufanisi kwa kila mwaka.

Kupitia maulid hayo Dk.Bashiru,aliwasihi Wazazi,Walezi na Viongozi mbali mbali wa Dini na Serikali kuwa karibu zaidi na Walimu wa Madrasa kwa kuwatimizia mahitaji yao ya msingi ili wanaendee kufundisha watoto kwa bidii kwani wengi wanajitolea.

Naye  Mwakilishi wa Jimbo la Tumbatu, Haji Omar Kheri aliwashukuru Wageni waalikwa kwa kuthamini hafla hiyo ya Maulid kwani ushiriki wao ni sehemu ya Umoja na Mshikamano wa Waumini wa Dini ya Kiislamu nchini.

Haji,alisema msikiti huo wa Gomani yanapofanyika maulid  una historia kubwa ya harakati za Ukombozi na Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964, kwani Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Sheikh Abeid Karume aliwasihi kufika katika Msikiti huo katika harakati za kufanya Mapinduzi ya kuondosha dhiki na dhuruma kwa Wananchi wa Visiwa vya Zanzibar.

Mapema Maelfu ya Waumini wa dini ya kiislamu na wananchi kwa ujumla walijitokeza katika bandari ya Tumbatu, kumpokea Katibu Mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ally aliyekuwa mgeni rasmi, ambaye yupo nchini kwa ajili ya ziara ya siku tisa (9) ya kikazi ya kuimarisha Chama Cha Mapinduzi.
KUONA PICHA ZA HAFLA HIYO/ BOFYA HAPA

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages