Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tayari limeipitisha rasmi sheria inayompa mamlaka, mtu kujipima mwenyewe Virusi vya Ukimwi kwa kutumia sampuli zinazotoka kwenye kinywa, pamoja na sheria inayoruhusu kijana kuanzia miaka 15, kupima Ukimwi bila ridhaa ya mzazi.
Sheria hiyo imepitishwa leo Novemba 12, 2019, na kwamba sheria hiyo itasaidia watu kujitambua hali zao mapema, hususani wanaume na kundi la vijana, ambalo kwa sasa ndilo linaloongoza kuwa na waathirika wengi wa ugonjwa huo.
Akizungumza bungeni Dodoma, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Faustine Ndugulile, amesema kuwa tayari Wizara imekwishajipanga juu ya upatikanaji wa vipimo hivyo na tayari imeshaanza kufanya majaribio ya mifumo hiyo ikiwa ni pamoja na kuangalia mapokea kutoka kwa wananchi.
"Vipimo hivi havitakuwa vinatumia damu, vitakuwa vinatumia sampuli ya kinywa na hii watu watapima hata kabla ya kujamiiana na watakapobaini wamepata changamoto hizo wanakuja katika vituo vya kutoa huduma za afya ili kujiridhisha,vijana wengi wameanza kuathirika na kujamiiana wakiwa na umri mdogo, sasa tunatoa fursa kwa vijana kuanzia miaka 15 kupima Ukimwi bila ridhaa ya mzazi wake" amesema Waziri Dkt Ndugulile.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇