Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stellah Manyanya akikata utepe kuashiria kuzindua Kitabu cha Siri za Mafanikio ya Ndoa katika hafla iliyofanyika juzi jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mtunzi wa Kitabu hicho, Mchungaji Dkt.Sako Mayrick na kushoto ni mke wake Mariam Sako.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stellah Manyanya akionesha kitabu hicho baada ya kukizindua.
Washiriki wa hafla hiyo wakipatiwa nakala ya kitabu hicho.
Washiriki wa hafla hiyo wakipatiwa nakala ya kitabu hicho.
Na Kulwa Mwaibale
NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Injinia Stella Manyanya, amesema watanzania wengi wanachangamoto za kindoa hali inayosababisha msongo wa mawazo, mdororo wa kiuchumi na jamii isiyo na malezi bora.
Ameongeza kuwa asilimia 90 ya ndoa hizo zimekufa na wenza wake wanaishi kwa maonyesho na dhana ya kuvumiliana wakiona aibu kutengana hivyo ipo haja kufanyika kwa tafiti na kuwekeza nguvu katika elimu ya ndoa.
Injinia Manyanya aliyasema hayo jana akizindua Kitabu cha Siri za mafanikio ya Ndoa kilichoandaliwa na mtunzi ambaye ni Mchungaji na Mkurugenzi wa Fedha wa Bohari ya Dawa
(MSD), Dk. Sako Mayrick.
Naibu Waziri huyo alisema watanzania wengi wanachangamoto za kindoa hali inayosababisha
msongo wa mawazo, mdororo wa kiuchumi na jamii isiyo na malezi bora.
“ Ni kawaida watu kufanya sherehe za ndoa na kutumia gharama kubwa lakini ndoa zinazoishi na hai ni chache huku nyingi kuvunjika kwake ni kimyakimya kwa dhana ya kuona
aibu,”alisema.
Alisema changamoto hizo ndio zinazochangia ongezeko la wagonjwa wa akili, baadhi ya watu kuwa na msongo wa mawazo uliopitiliza hadi kupasuka mishipa ya fahamu, gharama kubwa ikitumika kusafirisha baadhi ya wagonjwa nje ya nchi huku kiini cha matatizo ikiwemo ni
migogoro iliyokithiri ya kifamilia.
“Imefika wakati wasomi wetu kutumia uwezo wao katika kutoa elimu ya ndoa na familia, na kujua ndoa si fasheni tu, vitabu vya aina hii vinasahaulika hivyo iwe chachu ya kupambana na matatizo yaliyopo kwakuwa vita ya uimarishaji wa ndoa katika jamii inahitaji watu wa kiroho na kitaalamu wakiwemu wa ustawi ya jamii kushirikiana,” alisema.
Alisema utunzi wa vitabu hivyo pia ni fursa ya kuufikia uchumi wa kati wa viwanda hivyo alimpongeza Sako kuandika kitabu hicho alichosema kitaisadia kurejesha amani na upendo kwa watu wengi hususani vijana kutokana na mafunzo yaliyomo.
“Kama kitabu hiki kingeandikwa siku nyingi huko nyuma huenda nami kingenisaidia,” alisema.Alisema, kufuatia fursa zilizopo, uandishi wa vitabu ni ajira na uwekezaji katika viwanda vya uchapishaji hivyo amewashauri Watanzania kuandika kwa wingi vitabu vilivyosahaulika na vyenye uhitaji kwa jamii ili kuweza kuufikia uchumi wa kati wa viwanda.
Aliongeza kuwa ndoa zinapokuwa na amani familia zitakuwa na furaha hivyo kuweza kufanya kazi zenye tija jambo litakaloinua uchumi wa Taifa.
Naye Profesa Amos Mwakigonja kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), alimpongeza Sako ambaye licha ya kuwa mtumishi wa serikali ni mchungaji wa Kanisa la Mafanikio la Kikristo ambaye anatumia muda mwingi kuandika vitabu.
“Sisi wataalamu wa afya tunakutana na changamoto nyingi za watu waliothirika na matatizo ya kindoa, Sako ni mpambanaji, mwenye kutumia elimu yake ya uhasibu, sheria na huduma za kiroho kwa ajili ya jamii ni muhimu kuungwa mkono,” alisema.Kwa upande wake muandishi wa Kitabu hicho Dk. Sako alisema jamii imekuwa na changamoto nyingi za kindoa zinazosababishwa na mfumo dume.
Alisema ni muhimu kuelewa kuwa mwanamke katika ndoa si mtu aliyepo kwa ajili ya kuzaa, kufanya kazi za nyumbani na kulea familia pekee kwakuwa ana nguvu na uwezo wa kuharibu maisha iwapo wawili hao hawatathaminiana na kuishi kwa makubaliano.
“ Maisha ya ndoa bora ni muhimu sana hivyo wenza hawana budi kukubaliana baadhi ya mambo, ilichukua miaka kumi kujifunza kupitia vitabu, kufanya utafiti, semina na maandiko
matakatifu kuweza kuelewa maana ya ndoa na kusudio la Mungu katika kuishi kwa amani,” alisema.
Alieleza kuwa imefika wakati wa kujua tofauti kati ya ngono, mapenzi na tendo la ndoa kuwa inaweza leta mapinduzi makubwa katika jamii na uchumi.Alisema kupitia kitabu hicho watu watajifunza namna ya kupata mchumba bora, sifa 15 za mke na mume aliyebora, misingi 21 ya maisha ya wanandoa, heshima ya tendo la ndoa, nguvu na mamlaka ya mwanamke na athari za mitandao.
Mambo mengine alisema ni misingi ya sheria ya ndoa, miiko ya wanandoa katika uhusiano na maombi 100 kwa ajili ya uchumba hadi ndoa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇