Wafanyakazi sita wa masuala ya tiba na afya waliokuwa wametekwa nyara na watu wasiojulikana karibu wiki mbili zilizopita huko nchini Libya wameachiliwa huru.
Shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch lilithibitisha habari hiyo jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, madaktari wanne, nesi mmoja na mtaalamu mmoja wa masuala ya kiufundi waliachiliwa huru Jumatano. Hata hivyo uraia wa watu hao haukuweza kujulikana mara moja.
Shirika hilo la Human Rights Watch limeongeza kuwa, wafanyakazi hao waliokuwa wametekwa nyara walitumiwa kwa ajili ya kukombolewa mtu mmoja aliyekuwa amefungwa jela. Mtu huyo ametajwa kwa jina la Izzedine al Wahishi ambaye hivi sasa anashikiliwa katika jela moja mjini Tripoli.
mapigano

Hata hivyo mtandao wa habari wa Libya Observer umesema kuwa, watu hao wameachiliwa huru baada ya kutokea malalamiko makubwa kutoka kwa jamaa na marafiki zao pamoja na juhudi zilizofanywa na maafisa wa kieneo wa serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Libya haijawahi kuwa na utulivu wa angalau siku moja tangu alipopinduliwa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Muammar Gaddafi mwaka 2011.
Machafuko yameongezeka tangu mwezi Aprili mwaka huu baada ya jenerali muasi, Khalifa Haftar anayeungwa mkono na Saudi Arabia, Imarati, Misri na Ufaransa kuanzisha mashambulizi ya kila upande ya kutaka kuuteka mji mkuu Tripoli na kuipindua serikali ya Umoja wa Kitaifa inayotambuliwa kimataifa.
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇