Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
CHAMA
cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Hazina Saccos kimeazimia kujenga
kitega uchumi cha kisasa kwa gharamaya Shilingi bilioni 52 kupitia
mradi wa Njedengwa katika Jiji la Dodoma ili kukuza uchumi wa mkoa wa
Dodoma na Taifa kwa kupitia kodi.
Hayo
yamebainishwa leo Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi wa chama
hicho cha Ushirika Bw. Aliko Mwaiteleke wakati wa Mkutano Mkuu wa
Mwaka uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano Hazina, na kuongeza kuwa
mradi huo upo katika hatua za mwisho za utekelezaji wake.
Mwaiteleke
alisema mpaka sasa upembuzi yakinifu wa mradi huo utakaojengwa kwa njia
ya ubia kati ya Hazina Saccos na mwekezaji kwenye neo lenye ukubwa wa
ekari 22 kupitia utaratibu wa Jenga, Endesha na Hamisha (Build, Operate
and Transfer - BOT) ambapo mwekezaji atagharamia ujenzi wote na
kuendesha kwa muda ambao utakubaliwa ndani ya mkataba.
Alisema
mradi huo unasimamiwa na Kamati ya watu Saba wakiongozwa na Profesa
Esta Eshengoma kutoka Chuo Kiuu Cha Dar es Salaam na wajumbe wake kutoka
Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Bodi ya Manunuzi ya
Umma (PSPTB), Kituo Cha Uwekezaji (TIC), na Chuo Kikuu cha Ardhi ambao
kwa sasa wanafanya kazi ya kusaka mwekezaji ili kufanikisha mradi huo.
Bw.
Mwaiteleke alifafanua kuwa Mradi wa Njedengwa upo mbioni kuanza na
unategemewa kuwa chachu ya maendeleo ya chama hicho kwa kukiingizia
kipato kutokana na shughuli zitakazokuwa zikifanyika kupitia mradi huo.
Alifafanua
kuwa mradi huo utahusisha ujenzi wa hoteli ya kisasa, kumbi za
mikutano, majengo ya Ofisi, Viwanja vya Michezo na bwawa maalum la
kuogelea.
Aidha
alisema Chama hicho cha Hazina Saccos ambacho kina wanachama 5,600 kina
mtaji mtaji wenye thamani ya shilingi bilioni 10 ikiwa ni fedha taslimu
na mali wanazozimiliki ikiwemo ardhi ambazo zimekuwa na manufaa makubwa
kwa wanachama..
"Mwaka
jana pekee kupitia akiba na mikopo tulipata faida ya shilingi milioni
64 na kila mwanachama alipewa gawio la asilimia 20 kulingana na hisa
zake"alisema Mwaiteleke.
Alisema
faida nyingine waliyopata kupitia Hazina Saccoss ni kununua viwanja 150
katika maeneo mbali mbali ya mkoa wa Dar es Salaam na Pwani na
kuwakopesha wanachama wao kwa bei nafuu ambapo wanalipa kidogo kidogo
kwa miezi 60.
"Pia
Dodoma tumenunua viwanja 897 katika maeneo ya Ihumwa Ngaloni,
Iyumbu (maeneo ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ambavyo tumevigawa kwa
wananchi na viwanja vya Nzuguni tutaanza kuvigawa baada ya taratibu za
Halmashauri ya Jiji la Dodoma kukamilika ili kuwawezesha wanachama wetu
waliohamia Dodoma kupata maeneo ya kujenga makazi yao” alisema Bw.
Mwaiteleke
Naye
Meneja wa Hazina Saccos Bw. Festo Mwaipaja, alisema Saccoss hiyo sio ya
wafanyakazi wa Wizara ya Fedha peke yake bali watumishi wote wa serikali
wanaruhusiwa kujiunga na chama hicho isipokua vyombo vya ulinzi na
usalama ambavyo ni jeshi, Polisi, na Usalama wa Taifa.
Alisema
kwa mtumishi wa umma kujiunga na chama hicho cha ushirika mbali na kuwa
muajiriwa pia atapaswa kulipa kingilio cha shilingi 20,000 na kununua
hisa kuanzia 20 ambazo kila hisa moja ni shilingi 10,000 na kufanya
thamani ya hisa zote kuwa shilingi 200,000.
Aidha
alisema kuna mchango wa shilingi 20,000 kila mwezi na kuwataka watumishi
wa umma kutoka taasisi na idara zote za serikali kuchangamkia fursa ya
kujiunga na ushirika huo ili kujiinua kiuchumi
Kuhusu
viwanja, Bw. Mwaipaja alieleza kuwa Chama hicho kimetumia zaidi ya
shilingi bilioni 4 kununua viwanja katika Jiji la Dodoma na kuchangia
eneo hilo kuwa na mzunguko mkubwa wa fedha kwa wenyeji na kwamba hayo ni
mafanikio yanayoihusu jamii.
Akifungua
Mkutano Mkuu huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Mary
Maganga, ameipongeza Hazina Saccos kwa kuwapatia viwanja wanachama wake
na kuwataka wanachama waliopata fursa ya kupata viwanja hivyo
waviendeleze haraka ili kuodokana na changamoto ya malazi kwa kuwa
baadhi walipata viwanja hivyo tangu mwaka uliopita, 2018.
Aidha,
ameipata kongole Hazina Saccos kwa hatua waliyofikia ya kutafuta
mwekezaji katika mradi wa Njedengwa ambao utaongeza mapato ya Ushirika
na kuwataka viongozi na wanachama kuhakikisha wanazingatia taratibu
Sheria na Kanuni ili kufanikisha mradi huo muhimu.
Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Mary Maganga, akizungumza
jambo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Ushirika wa Akiba na
Mikopo cha Hazina Saccos leo jijini Dar es Salaam,ambapo amekipongeza
chama hicho kwa kuwapatia viwanja wanachama wake na kuwataka waliopata
viwanja hivyo waviendeleze.
Mwenyekiti
wa Bodi wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Hazina Saccos,Bw.
Aliko Mwaiteleke akifafanua jambo mbele ya Wanachama waliohudhuria
mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama hicho uliofanyika kwenye ukumbi wa
mikutano Hazina, leo jijini Dar es Salaam.
Meneja
wa Hazina Saccos Bw. Festo Mwaipaja akiwasilisha taarifa ya utekelezaji
ya majukumu ya Saccos hiyo kwa wajumbe wa mkutano Mkuu wa mwaka wa
chama hicho jijini Dar es Salaam.
Baadhi
ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha
Hazina Saccos wakifuatilia yaliyokuwa yakijadiliwa wakati wa Mkutano
huo uliofunguliwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi.
Mary Maganga (hayupo pichani).
Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Mary Maganga wa nne kushoto
akiwa katika picha ya pamoja na Sekretarieti ya bodi ya Hazina Saccos
baada ya kufungua Mkutano Mkuu wa Chama hicho cha Ushirika jijini Dar es
Salaam.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango).
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇