Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, ameipa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA miezi miwili na nusu hadi ifikapo Disemba 31 mwaka 2019, kuandaa na kuwasilisha wizarani orodha ya walipakodi, idadi ya majengo na mabango yote yaliyoko katika mkoa wa Dar es Salaam ili kupata takwimu sahihi za idadi ya walipakodi.
Dkt. Kijaji ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam alipofanya ziara ya kikazi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Mkoa wa Kikodi wa Temeke ili kukagua utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hayo ili kubaini fursa na changamoto za masuala ya ukusanyaji kodi.
Amesema kuwa pamoja na Mamlaka hiyo kufanya vizuri katika makusanyo ya mapato Mwezi Septemba, 2019, ambapo kiasi cha shilingi trilioni 1.78 kimekusanywa, kiasi hicho bado ni kidogo ikilinganishwa na mwamko wa wananchi uliopo hivi sasa katika kulipa kodi.
Aidha Mhe. Kijaji amerejea kuitaka TRA kuwasilisha kwake takwimu ya ongezeko la walipa kodi lililotokana na zoezi la kugawa vitambulisho vya wajasiriamali nchini kwa kuwa lengo la Mhe. Rais Dkt. John Magufuli kugawa vitambulisho hivyo lilikuwa ni kuongeza wigo wa walipa kodi watakao kuwa wanafuzu kwa kuongeza mitaji yao, hivyo ni vyema kujua idadi yao kamili na mahali walipo.
Kwa upande wa kodi ya majengo, Dkt. Kijaji ameitaka Mamalaka ya Mapato Tanzania kuhakikisha inapata orodha ya nyumba zote nchini kwa kuorodhesha wamiliki wa nyumba hizo na mawasiliano yao na kisha kuandaa kanzidata itakayosaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi hiyo.
“Ili kuongeza mapato yanayotokana na kodi ya majengo ni lazima TRA wafanye kazi usiku na mchana kuhakikisha kanzidata hiyo inakamilika ambayo itatumika kuwakumbusha walipa kodi kupitia ujumbe mfupi wa simu ambapo itasaidia katika ukusanyaji wa kodi hiyo kama ilivyo kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inapowakumbusha wananchi kulipa kodi a ardhi kupitia simu zao” Alisema Dkt. Kijaji
“Nataka pia mkague watumiaji wote wa mashine za utoaji risiti za kieletroniki (EFD) kwa wafanyabiashara wa Temeke ili kuhakikisha kila anayeuza anatoa risiti na anayenunua anadai risiti na kwa kufanya hivyo itasaidia kuongeza makusanyo ili Taifa liendelee kujitegemea kimapato” alisisitiza Dkt. Kijaji
Awali akimkaribisha Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Mkoa wa Kikodi wa Temeke, Bw. Paul Walalaze, alisema mkoa wake una idadi ya walipakodi 437,539 na kwamba katika mwaka 2018/19, mkoa wake ulipanga kukusanya shilingi bilioni 395 na kufanikiwa kukusanya sh. bilioni 328.5 sawa na asilimia 85 ya lengo.
“Tumekusanya pia kodi ya majengo sh. bilioni 1.4 kati ya malengo ya kukusanya bilioni 1.6, kodi ya mabango sh. bilioni 2.2 kati ya lengo la kukusanya sh. bilioni 2.3 sawa na mafanikio ya asilimia kati ya 87 na asilimia 95" aliongeza Bw. Walalaze.
Kwa upande wake Afisa Mwandamizi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Bw. Hamisi Lupenja, amemhakikishia Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Kijaji kwamba watatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa ili kuboresha ukusanyaji wa mapato ya Serikali ikiwemo kutoa elimu kwa walipakodi.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), katikati, akikagua kanzidata ya walipakodi wa majengo na mabango, katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, mkoa wa Kikodi wa Temeke Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Bi. Hellen Gibbe Msimamizi Msaidizi wa Kodi na kushoto ni Msimamizi wa Kitengo cha Mapato yasiyo ya Kodi, wote kutoka TRA-Temeke.
Mkuu wa masuala ya usimamizi wa Data na Ukaguzi wa ritani Bw. Pius Kunjumu (aliyesimama nyuma) akitoa ufafanuzi wa jambo kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango (Hayupo pichani) alipofanya ziara katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Mkoa wa Kikodi wa Temeke, Jijini Dar es Salaam, kusikiliza fursa na changamoto ya utendaji kazi wa Mamlaka hayo ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji kodi.
Meneja Msaidizi wa Kitengo cha Madeni wa TRA-Temeke, Bw. Nicholaus Migera, (aliyesimama) akitoa ufafanuzi wa jambo kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango (Hayupo pichani) alipofanya ziara katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA Mkoa wa Kikodi wa Temeke, Jijini Dar es Salaam, kusikiliza fursa na changamoto ya utendaji kazi wa Mamlaka hayo ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji kodi.
Afisa Mwandamizi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Bw. Hamisi Lupenja akifafanua jambo mbele ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (hayupo pichani) alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi hizo za TRA Mkoa wa Kikodi wa Temeke Jijini Dar es Salaam.
Afisa Mwandamizi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Bw. Hamisi Lupenja (kulia) na Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Mkoa wa Kikodi wa Temeke, Jijini Dar es Salaam. Bw. Paul Walalaze, wakisikiliza hoja za watumishi wa TRA-Temeke, Jijini Dar es Salaam wakati Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (hayupo pichani) alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi hizo.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), akisikiliza kwa makini hoja mbalimbali za watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Ofisi ya Temeke (hawapo pichani), alipotembelea Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Mkoa wa Kikodi wa Temeke, Jijini Dar es Salaam
Katibu wa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), Bw. Moses Dulle, akitoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo wakati Dkt. Kijaji aliofanya ziara ya kikazi kukagua utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, Mkoa wa Kikodi wa Temeke, Jijini Dar es Salaam
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇