Shirika la Afya Duniani (WHO) limeipati Uganda msaada wa dozi 300 za chanjo ya Ebola kwa ajili ya kuwapatia chanjo watu wote waliowasiliana na msichana mwenye umri wa miaka 9 aliyefariki dunia kutokana na ugonjwa wa Ebola katika wilaya ya Kasese inayopakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mwakilishi wa WHO nchini Uganda, Yonas Tegegn Woldemariam, amewaambia wanahabari kuwa chanjo hiyo itatumika kwa wale wote waliowasiliana na kumhudumia mtoto huyo katika kitengo cha matibabu ya Ebola cha hospitali ya Bwire.
Kwa mujibu wa Waziri wa Afya wa Uganda Joyce Moriku Kaducu, watu wanne waliosafirishwa kwenye gari moja ya wagonjwa na mtoto huyo wamesharejeshwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ili kupewa chanjo na kufuatiliwa zaidi.
Tayari watu zaidi ya 200,000 wamepata chanjo ya ugonjwa hatari wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mwezi huu wa Agosti.
Taarifa iliyotolewa wiki iliyopita na serikali ya DRC ilisema inatumai kuwa chanjo hiyo utaweza kukabiliana na mlipuko wa sasa wa Ebola ambao ni wa pili kwa maangamizi katika historia ya ugonjwa huo.
Kwa ujumla ugonjwa hatari wa Ebola umeua watu 2000 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika kipindi cha mwaka moja uliopita na bado ugonjwa huo haujadhibitiwa huku kukiwa na hatari ya kuenea katika nchi jirani.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇