WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka vijana na jamii kwa ujumla wasikwepe jukumu la kuwatunza wazee kwa sababu nguvu zao za uzalishaji mali zimepungua kutokana na kazi waliyoifanya wakiwa vijana kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa familia zao na Taifa kwa ujumla.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kutokomeza Mauaji ya Wazee uliozinduliwa Januari, 2019 ili kwa kutokomeza ukatili kwa wazee ifikapo 2023 na kuhakikisha wazee na watu wenye ulemavu wanatambuliwa na kulindwa dhidi ya ubaguzi, uonevu, ukatili na mila potofu.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumapili, Septemba 29, 2019) wakati akizindua kambi ya utoaji wa huduma za afya kwa wazee na watu wenye ulemavu katika viwanja vya Kichanganimjini Iringa. Kambi hiyo imeandaliwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Dkt. Ritta Kabati katika kuadhimisha siku ya Wazee Duniani.
Amesema wajibu wa kuwahudumia au kuwasaidia wazee na watu wenye ulemavu ni wa kila mmoja na wanapaswa watambue kwamba wazee hao wamelitumikia Taifa kwa muda mrefu tena kwa namna mbalimbali ikiwemo kuwaletea na kuhakikisha wanapata mafanikio hayo ambayo wanajivunia sasa.
“Kwa msingi huo, tunao wajibu wa kuwajali wazee wetu kwa hali na mali ikiwa ni sehemu ya matunda ya uwajibikaji wao kwetu na kwa Taifa kwa ujumla. Hivyo basi, tutumie vema Kambi hii kuwasaidia wazee wetu na watu wenye ulemavu kwa kutambua afya zao na kuwapatia matibabu ya kiafaya ili waendelee kuwa salama na wenye furaha nasi tuvune busara zao.”
Kutokana na umuhimu wa kuwatunza wazee na kuwasaidia watu wenye ulemavu, Waziri Mkuu ametoa rai kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa, wananchi na wadau mbalimbali kuendelea kuimarisha upatikanaji wa fursa, haki na ustawi wa wazee ikiwemo kuondokana kabisa na vitendo vya ukatili dhidi yao.
“Vituo vyote vya kutoa huduma za afya vya umma kutoa huduma bora na za haraka kwa wazee wetu wenye vitambulisho. Tengeni dirisha maalumu kwa ajili ya kuwahudumia ili wasikae kwenye foleni muda mrefu. Serikali itaendelea kuweka miundombinu na mazingira rafiki ili kuwawezesha kupata mahitaji yao.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kusimamia maelekezo yake kwa Halmashauri zote nchini kuwatambua wazee wasiojiweza na kuwapatia vitambulisho vya matibabu bila malipo. “Namshukuru Mbunge wa Viti Maalum Ritha Kabati amebainisha mafanikio yanayoendelea kupatikana kutokana na utekelezaji wa agizo hilo.
“Haidhuru nasi tukiiga mfano wa Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalumu na kaka yangu Mheshimiwa Pinda, Waziri Mkuu Mstaafu kwa moyo wao wa kizalendo kabisa kuona kuna haja ya kusaidia na kuunga mkono juhudi za Rais wetu mpendwa Dkt. John Magufuli za kuwahudumia wanyonge.”
Hata hivyo, Waziri Mkuu ameendelea kuziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha zoezi hilo linakuwa endelevu kwa kuwatambua na kuwapatia vitambulisho wazee wote nchini wasio na uwezo ili waweze kunufaika na huduma ya matibabu bila malipo pamoja na huduma zingine za kijamii.
Vilevile, Waziri Mkuu amesema kwa kuwa Novemba 2019 nchi inatarajia kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, wazee kama sehemu ya jamii wana haki ya kushiriki katika uchaguzi huo kwa kuchagua viongozi wanaoona watafaa kuwaongoza na wao kuchaguliwa kuongoza katika nafasi mbalimbali. Hivyo wasaidiwe kushiriki zoezi hilo.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Mstaafu na Mlezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa, Peter Pinda alimpongeza Dkt. Ritta kwa uamuzi wake wa kuandaa kambi hiyo ambayo itatoa fursa kwa wazee kupima afya zao na kupatiwa huduma pamoja na kutoa viungo bandia kwa baadhi ya walemavu.
“Uzee ni hali siyokwepeka upende usipende ila unaweza kucheleweshwa kutegemea na aina ya matunzo wanayopatiwa. Nashauri wazee wapate vyakula bora tena kwa uwiano sahihi, vyakula hivyo ni pamoja na vya jamii ya mizizi, mikunde, nafaka, mbogamboga na nyama ili waweze kuimarisha afya zao.”
Awali, Waziri Mkuu alipokea taariza za ujenzi wa jengo la Ustawi wa Jamii Manispaa ya Iringa lilojengwa kwa ufadhili wa Mkurugenzi wa Kundi la Makampuni ya Asas, Salim Abri kwa gharama ya sh. milioni 60.
Kwa upande wake,Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Iringa Tiniel Mmbaga alisema kukamilika kwa jengo hilo kutawawezesha kutoa huduma bora kwa jamii na kwa wakati kwani awali maafisa watano walikuwa wakilundikana katika chumba kimoja hali iliyosababisha wateja kushindwa kueleza matatizo yao baada ya kukosekana kwa usiri.
Alisema kwa siku wanashughulikia malalamiko yahusuyo masuala ya migogoro ya familia ikiwemo matunzo ya watoto kuanzia 15 hadi 30 pamoja na wanawake zaidi ya 50 ambao kila mwezi wanakwenda kuchukua fedha kwa ajili ya matunzo ya watoto zinazotolewa na wenza wao kufuatia kuwepo kwa migogoro baina yao.
Shughuli hiyo, imehudhuriwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Augustine Mahiga, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- TAMISEMI Josephat Kandege, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na wenye UlemavuStela Ikupa pamoja na Maafisa wengine wa Serikali.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda wakati alipowasili kwenye uwanja wa Kichangni Kihesa mjini Iringa kuzindua Kambi ya Kutoa Huduma za Afya kwa Wazee na Walemavu, Septemba 29, 2019. Wa pili kushoto ni Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa na wa pili kulia ni Mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wazee wakati alipozindua Kambi ya Kutoa Huduma za Afya kwa Wazee na Wenye Ulemavu kwenye Uwanja wa Kichangani Kihesa mjini Iringa, Septemba 29, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akislimiana na Bibi Costancia Alfred Mapunda wakati alipozindua Kambi ya Kutoa Huduma za Afya kwa Wazee na Wenye Ulemavu kwenye Uwanja wa Kichangani Kihesa mjini Iringa, Septemba 29, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakizungumza na wazee waliojitokeza kupata huduma za tiba na vipimo wakati Waziri Mkuu alipozindua Kambi ya Kutoa Huduma za Afya kwa Wazee na Wenye Ulemavu kwenye Uwanja wa Kichangani Kihesa mjini Iringa, Septemba 29, 2019.
Baadhi ya wazee wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozindua Kambi ya Kutoa Huduma za Afya kwa Wazee na Wenye Ulemavu kwenye Uwanja wa Kichangani Kihesa mjini Iringa, Septemba 29, 2019.
Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa akisalimiana na Mbunge wa Viti Maalum, Ritta Kabati na baadhi ya viongozi wa CCM walioshiriki katika uzinduzi wa Kambi ya Kutoa Huduma za Afya kwa Wazee na Wenye Ulemavu kwenye Uwanja wa Kichangani Kihesa mjini Iringa, Septemba 29, 2019
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Happi akizungumza wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipozindua Kambi ya Kutoa Huduma za Afya kwa Wazee na Wenye Ulemavu kwenye Uwanja wa Kichangani Kihesa mjini Iringa, Septemba 29, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Tuzo ya Shukurani, Mkurugenzi Mkuu wa Makmpuni ya ASAS, Salim Abri kutokana na mchango wake mkubwa katika huduma mbalimbali za jamii mkoani Iringa. Tuzo hiyo imetolewa na Halmashauri ya Mji wa Iringa. Wa pili kushoto ni Waziri Mkuu Mstaafu na Mlezi wa CCM Mkoa wa Iringa, Mizengo Pinda, wa pili kulia ni Naibu Waziri Ofis ya Waziri Mkuu, Stella Ikupa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wazee wakati alipozindua Kambi ya Kutoa Huduma za Afya kwa Wazee na Wenye Ulemavu kwenye Uwanja wa Kichangani Kihesa mjini Iringa, Septemba 29, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇