Kufuatia hatua ya Uturuki ya kununua mfumo wa makombora wa S-400 kutoka Russia, wakuu wa nchi hiyo sasa wameazimia kununa ndege za kisasa za kivita za Russia za Sukhoi-35 na Sukhoi-57.
Kuhusiana na hilo, Rais Reccep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesisitiza kuhusu kuendeleza jitihada za kununua ndege za kivita za Russia na kusema: "Uturuki inakusudia kununua ndege za kivita za Russia aina ya Sukhoi Su-35 na Sukhoi Su-57."
Iwapo Uturuki itaweza kununua ndege hizo za kisasa kabisa za kivita kutoka Russia basi tunaweza kusema kuwa: "Uturuki sasa imeanza kubadilika na kuwa mshirika wa karibu wa Russia katika kanda hii licha ya kuwa ni mwanachama wa muungano wa kijeshi uanongozwa na Marekani unaojulikana kama Shirika la Mkataba wa Atlantiki ya Kaskazini (NATO).
Pamoja na hayo Rais Erdogan wa Uturuki amesema kuwa kununua silaha za Russia kuna lengo la kudhamini usalama wa nchi hiyo. Aidha amesisitiza kuwa Uturuki itaendelea kuwa mwanachama wa NATO
Weledi wa mambo wanasema sambamba kuimarisha zaidi ushirikiano wa kijeshi na Russia, hivi sasa Uturuki imeanza kujitenga na washirika wake wa jadi, yaani Marekani na Umoja wa Ulaya.
Kuhusiana na hili, wataalamu wa mambo ya kijeshi wanasema kuwa, viwango vizuri vya silaha za Russia ikiliganishwa na viwango vya silaha za Marekani ni moja ya sababu ambayo imeifanya Uturuki kuegemea zaidi upande wa Russia katika masuala ya ulinzi.
Kwa mfano, Kanali Viktor Litovkin, mtaalamu wa masuala ya kijeshi analingani mfumo wa makombora ya kujihamu wa S-400 wa Russia na ule wa Patriot wa Marekani na kusema: "Mfumo wa S-400 unahesabiwa kuwa kati ya mafanikio makubwa zaidi ya viwanda vya kijeshi nchini Russia. Hii ni silaha ya kisasa kabisa. Hakuna nchi yeyote duniani imeweza kumiliki silaha kama hii. Marekani pia, ambayo inapigia debe na kuuza silaha zake kote duniani haijaweza kuunda silaha kama hii. Mfumo bora zaidi wa kujihami angani wa Marekani ni ule wa Patriot PAC-3 ambao hata hauwezi kuliganishwa na ule mwingine wa Russia wa S-300 seuze S-400."
Ikumbukwe kuwa mapema mwezi Julai, Uturuki ilianza kupokea shehena ya kwanza ya mfumo wa makombora wa S-400 kutoka Russia licha ya makelele na vitisho vya Marekani. Mkataba wa mauzo ya ngao hiyo ya makombora kati ya Ankara na serikali ya Moscow ulitiwa saini Disemba mwaka 2017.
Tunaweza kusema kuwa, hatua ya serikali ya Uturuki kununua silaha bora na zenye viwango vya juu za Russia ni njia mojawpao ya kujikomboa kutoka katika utumwa wa kununua silaha duni kutoka Marekani.
Baada ya Uturuki kununua mfumo wa kujihami angani wa S-400 kutoka Russia, Wizara ya Ulinzi ya Marekani ilitangaza kubatilisha mkataba wa kuiuzia Uturuki ndege za kivita za kizazi cha tano aina ya F-35. Aidha baada ya Uturuki kupokea mfumo wa S-400, Bunge la Marekani, Kongress, ya Marekani ilitangaza kuunga mkono hatua hiyo ya kubatilishwa mkataba wa kuiuzua Uturuki ndege hizo za kivita. Marekani imechukua uamuzi huo pamoja na kuwa Uturuki ilikuwa imelipa malipo yote yaliyohitajika kununua ndege 116 za kivita aina ya F-35. Kufuatia hatua hiyo ya ukiukaji mkataba, kumeibuka ufa mkubwa kati ya Marekani na mshirika wake mkuu katika eneo la Asia Magharibi na inatarajiwa Uturuki itapunguza kiwango cha ushiriki wake kijeshi katika muungano wa NATO.
Kilicho wazi ni kuwa maamuzi ambayo Uturuki imechukua ni magumu na nyeti na yamkini madola ya Magharibi yanapanga njama ya kuipa pigo serikali ya rais Erdogan.
Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, uamuzi wa wakuu wa Uturuki kununua silaha kutoka Russia, kutakuwa mwanzo wa kumalizika jitihada za zaidi ya miongo sita za ushirikiano wa Uturuki na nchi za Magharibi.
Kilichowazi ni kuwa, hivi sasa Uturuki imeacha kuwa mshirika wa Magharibi na sasa inaelekea upande wa Russia, nchi ambayo inatazamwa na NATO kama hasimu mkubwa. Inafaa kutaja hapoa kuwa, kubadilika muelekeo wa Uturuki kunatokana na sera zisizo sahihi za Rais Donald Trump wa Marekani.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇