LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 8, 2019

SAUDIA NA MIKAKATI YA KUANZISHA SERIKALI NYINGINE KUSINI MWA YEMEN

Hatua hiyo inachukuliwa baada ya Saudia na washirika wake kukwama katika kinamasi cha Yemen. Kwani utawala huo wa kifalme na washirika wake wameshindwa kuiangamiza harakati ya Ansarullah na kinyume chake, kundi hilo la wanamapambano wa Yemen limepata nguvu zaidi na kudhibiti sehemu kubwa ya nchi hiyo ukiwemo mji mkuu, Sana'a; na katika upande mwingine vita vya niaba baina ya mamluki na vibaraka wa Riyadh na Abu Dhabi katika maeneo ya kusini mwa Yemen vimesababisha maafa makubwa na kudhihirsha mgawanyiko na hitilafu kubwa zinazotawala muungano huo. 
Wachambuzi wa mambo wanasema Saudi Arabia ambayo imekata tamaa ya kuweza kuishinda harakati ya Ansarullah na washirika wake na hatimaye kumrejesha madarakani kibaraka na mwanasesere wake, Abdrabbuh Mansur Hadi, inafanya kila iwezalo kuhakikisha kwamba, inadhibiti mgogoro wa sasa kusini mwa Yemen na kuzuia kuundwa serikali nyingine. Kwa msingi huo Aal Saud wameualika mara mbili ujumbe wa Baraza la Mpito la Kusini unaoongozwa na gavana wa zamani wa Aden, Meja Jenerali Aidarus al-Zoubaidi, na kumtaka asiunde serikali wala kuzidisha mapigano na serikali iliyojiuzulu ya Mansur Hadi. 
Raia hususan watoto wa Yemen wanaendelea kuwa wahanga wa vita vya Saudia.
Inaonekana kuwa, matokeo ya mikutano na mazungumzo ya pande hizo mbili yalikuwa kushirikishwa Baraza la Mpito la Kusini linalofadhiliwa na Imarati katika serikali kibaraka ya Abdrabbuh Mansur Hadi. Mfichuaji wa siri za utawala wa kifalme wa Saudi Arabia anayejulikana kwa jina la Mujtahjid anasema: "Muhammad bin Salman amemuahidi Mansur Hadi kwamba atamrejeshea maeneo aliyokuwa akidhibiti huko Aden na miji mingine kwa sharti kwamba, alishirikishe Baraza la Mpito la Kusini katika serikali yake badala ya wanachama wa chama wa al Islah." 
Mwenendo huu wa Bin Salman unaashiria nukta kadhaa muhimu kuhusiana na hali ya kusini mwa Yemen: 
Kwanza ni kwamba mrithi wa ufalme wa Saudia analazimika kufanya mapatano na Imarati na wapiganaji wa Baraza la Mpito la Kusini, na takwa lake la kushirikishwa baraza hilo katika serikali ya Mansur Hadi lina maana ya kushindwa Riyadh mkabala wa Abdu Dhabi.
Pili ni kwamba, Abdrabbuh Mansur Hadi na serikali yake iliyotoroka nchi ni mtekelezaji wa siasa za Saudi Arabia na wala si kiongozi huru anayechukua maamuzi yeye mwenyewe. Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, katika wiki za hivi karibuni Abdrabbuh Mansur Hadi amekuwa akitangaza upinzani wake waziwazi dhidi ya Baraza la Mpito la Kusini lakini sasa na chini ya mashinikizo ya serikali ya Riyadh, analazimika kulishirikisha baraza hilo katika serikali yake.
Mansur Hadi na Bin Salman
Tatu ni kwamba, serikali itakayoundwa huko Aden kwa kushirikisha Baraza la Mpito la Kusini na kambi ya Abdrabbuh Mansur Hadi itakuwa serikali isiyo na mlingano wala uwiano; hii ni kwa sababu mbali na pande hizo mbili kuwa wapinzani wa jadi, vilevile Baraza la Mpito linataka kujitenga eneo la kusini mwa Yemen na kuundwa nchi nyingine huru.
Nne ni kwamba, kutupiliwa mbali chama cha al Islah na kufukuzwa katika serikali ya Abdrabbuh Mansur Hadi kuna maana ya kujitokeza hitilafu kubwa huko kusini mwa Yemen, kwani chama hicho kina uchawishi mkubwa na nafasi muhimu baina ya watu wa kusini mwa nchi hiyo.
Kwa kutilia maanani haya yote tunaweza kusema kuwa, mashinikizo ya Saudi Arabia dhidi ya Abdrabbuh Mansur Hadi kwa shabaha ya kulishirikisha Baraza la Mpito la Kusini katika serikali yake yanatayarisha uwanja wa kujitokeza changamoto mpya na kuzidisha matatizo ya Saudi Arabia na Imarati huko Yemen.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages