Rwanda na Uganda kwa mara nyingine tena zimesisizia umuhimu wa kufungamana na Makubaliano ya Luanda yanayozitaka nchi mbili hizo jirani zijizuie na vitendo vyovyote vya uhasama.
Katika kikao na waandishi wa habari mjini Kigali akiwa pamoja na Sam Kutesa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe amesema kuwa, "Tumeafikiana kushughulikia masuala yenye utata kati yetu ndani ya siku 30, na kisha kamisheni husika itakutana katika mji mkuu wa Uganda, Kampala kutathmini hatua zilizopigwa."
Hali kadhalika Rwanda imetoa orodha ya raia wake wanaozuiliwa nchini Uganda ambapo Kampala imeahidi kushughulikia majina hayo kupitia mchakato wa kisheria na kuwaachia huru wale ambao hawatapatikana na ushahidi wa kuwatia hatiani.
Tarehe 21 ya mwezi uliopita wa Agosti, Marais Yoweri Museveni wa Uganda na Paul Kagame wa Rwanda walisaini makubaliano ya amani katika mji mkuu wa Angola, Luanda yenye lengo la kumaliza uhasama na mzozo uliopo baina ya mataifa hayo mawili jirani.
Marais hao walifikia makubaliano hayo katika mkutano wa pili huko Luanda mbele ya marais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Angola na Congo Brazaville waliokuwa wapatanishi katika mgogoro huo.
Joto la mzozo baina ya Rwanda na Uganda limekuwepo tangu mwanzoni mwa mwaka huu na limeathiri maisha ya watu kijamii na kiuchumi katika mataifa hayo jirani.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇