Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa vikali tuhuma zilizotolewa na Ujerumani, Uingereza na Ufaransa kuwa eti Iran ilihusika katika mashambulizi yaliyolenga kituo kikubwa cha kusafisha mafuta cha Aramco nchini Saudi Arabia na kusisitiza kuwa, madai hayo haya msingi wowote.
Rais Rouhani alisema hayo jana Jumatatu katika mazungumzo yake na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, pambozini mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York na kueleza bayana kuwa, "Madai hayo ni mchezo wa lawama usiokuwa na msingi wowote wala mashiko."
Aidha amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka amani na usalama katika eneo na kwamba kilichofanyika Saudia, ni jibu la Wayemen kwa mauaji na mashambulizi ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Riyadh dhidi yao.
Mapema jana, viongozi wa nchi hizo tatu za Ulaya, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Chansela wa Ujerumani Angela Merkel na Waziri Mkuu wa Uingereza, Borris Johnson walitoa taarifa ya pamoja iliyoibebesha dhima Iran kwa mashambulizi hayo ya Septemba 14, na kusisitiza kuwa wanaunga mkono uchunguzi unaoendelea juu ya hujuma hizo.
Hii ni katika hali ambayo, kikosi cha drone cha jeshi na wapiganaji wa kujitolea wa Yemen kimetangaza kuwa ndicho kilichohusika na shambulio dhidi ya vituo vya mafuta vya shirika la mafuta la Aramco katika viwanda vya kusafisha mafuta vya Abqaiq na Khurais vilivyoko mashariki ya Saudi Arabia.
Msemaji wa Jeshi la Yemen, Jenerali Yahya Sare'a alisema oparesheni hiyo ilifanyika katika fremu ya haki ya kisheria ya watu wa Yemen kujibu jinai za muungano wa kijeshi wa Saudia dhidi ya Yemen.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇