Mgogoro wa kidiplomasia umezuka baina ya Afrika Kusini na Nigeria baada ya magenge ya watu kushambulia wageni huko Afrika Kusini, na matokeo yake wananchi wa Nigeria nao kushambulia vituo vya biashara vinavyomilikiwa na raia wa Afrika Kusini nchini mwao.
Jana Alkhamisi, serikali ya Afrika Kusini ilitangaza kufunga kwa muda ubalozi wake mjini Abuja na ubalozi wake mdogo mjini Lagos baada ya wananchi wa Nigeria kuvamia na kushambulia vituo vya kibiashara vya raia wa Afrika Kusini, ili kulipiza kisasi cha kushambuliwa Wanigeria huko Afrika Kusini.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini imesema kuwa serikali ya Pretoria imeamua kufunga kwa muda ofisi zake za kibalozi nchini Nigeria, kutokana na hatari ya kutokea ulipizaji kisasi zaidi dhidi ya raia wa Afrika Kusini huko Nigeria.
Katika upande mwingine, Nigeria imetangaza kuwa itamwita nyumbani balozi wake aliyeko nchini Afrika Kusini baada ya raia wa kigeni kuanza kushambuliwa nchini humo.
Waziri wa Habari wa Nigeria, Lai Mohammed amewaambia waandishi wa habari mjini Abuja kwamba, Nigeria itamwita nyumbani balozi wake aliyeko Afrika Kusini na badala yake itatuma mjumbe maalumu kwennda kuonana na kuzungumza na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini.
Itakumbukwa kuwa jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Naledi Pandor, alisema kuwa tabia ya kujichukulia sheria mkononi dhidi ya raia wa nchi nyingine za Afrika wanaoishi nchini humo ni moja ya sababu za mashambulizi na hujuma zinazowalenga wafanyabiashara wa nchi za kigeni katika miji mbalimbali ya nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇