Afisa mmoja wa jeshi la anga la Marekani amesema kuwa Washington imetuma ndege zake za kiistratijia za B-2 nchini Uingereza kama njia ya kuonesha kuwa iko pamoja na serikali ya nchi hiyo.
Itakumbukwa kuwa, watu wanaopinga Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya (EU) wanasema kuwa, iwapo London itajitoa kwenye umoja huo basi itakuwa kibaraka wa Marekani.
Kanali Kurt Vendetti, mmoja wa maafisa wa jeshi la anga la Marekani ameiambia televisheni ya ITV kwamba ndege tatu za kiistratijia za jeshi hilo aina ya B-2 zimepelekwa kwenye kambi ya kijeshi ya Fairford, kusini mwa UIngereza na jambo hilo linatoa ujumbe maalumu wa kijeshi kwamba Marekani na waitifaki wake ikiwemo Uingereza wana uwezo wa kukabiliana kijeshi na maadui wakati wowote ule.
Ikumbukwe pia kuwa, gharama za saa moja tu za kuruka ndege hizo ni dola laki moja na 70 elfu za Kimarekani. Jeshi la Anga la Marekani lina ndege 20 tu za aina hiyo.
Afisa huyo wa jeshi la anga la Marekani amesema kuwa, ndege hizo zitakuweko nchini Uingereza kwa muda wa miezi miwili, na huo utakuwa ni muda mrefu zaidi kuwahi kuweko ndege za kivita za Marekani nchini Uingereza. Katika upande wingine, Marekani imeongeza uwepo wake kwenye mipaka ya Russia katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.
Russia nayo inatumia mbinu mbalimbali kulinda usalama wa mipaka yake kama vile kufanya mazoezi ya mara kwa mara ya kijeshi na kurusha angani ndege za kijasusi kuangalia kwa karibu harakati za Marekani na NATO katika mipaka yake hiyo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇