Madaktari wanaoendelea na mgomo nchini Zimbabwe wameeleza kuwa wamepokea vitisho vya kuuawa huku maafisa usalama wa taifa wakiwashinikiza baada ya polisi kuzuia maandamano yao ya pili jana Jumatano.
Madaktari hao walitaka kufanya maandamano hayo kulalamikia kupotea kwa kiongozi wa muungano wa madaktari nchini Zimbabwe.
Peter Magombeyi Mwenyekiti wa Muungano wa Madaktari wa Hospitali za Zimbabwe ( ZHDA) na ambaye pia ni muandaaji wa mgomo wa matabibu unaoendelea sasa nchini humo kudai nyongeza kubwa ya mishahara kwa madaktari wa hospitali za serikali alitoweka tangu Jumamosi usiku iliyopita. Madaktari hao wamesema wameamua kufanya mgomo ili kushinikiza kupandishiwa mishahara yao kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.
Owen Ncube Waziri wa Usalama wa Zimbabwe amesema kuwa serikali inashughulikia kesi ya Mwenyekiti wa Muungano wa Madaktari wa nchi hiyo kama kesi nyingine ya kawaida inayohusiana na mtu kutoweka na si utekaji nyara kama inavyodaiwa na madaktari wenzake. Makumi ya polisi wa kutuliza ghasia jana Jumatano waliwazuia madaktari zaidi ya 200 waliokuwa wakifanya juhudi za kuelekea bungeni kuwasilisha malalamiko yao huku wakipiga nara ya "hakuna Peter, hakuna kazi."
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇