Waziri wa Madini Doto Biteko (wa pili kulia), Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainabu Taleck ( katikati), Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (wa kwanza kulia) na Afisa Madini Mkoa wa Kimadini Kahama, Mhandisi Joseph Kumburu wakiangalia baadhi ya Kaboni inayochenjuliwa katika Kituo cha Kuchenjua Dhahabu cha Jema Afrika.
Afisa Madini Mkoa wa Kimadini Kahama, Mhandisi Joseph Kumburu akizungumza jambo wakati wa ziara ya Waziri wa Madini Doto Biteko katika kituo cha Kuchenjua Dhahabu cha Jema Afrika. Wengine wanaosikiliza ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainabu Tacleck na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo .
Waziri wa Madini Doto Biteko, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainabu Taleck, Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko wakiteta jambo na Kamati ya Ulinzi na Usalama mara baada ya kukitembelea Kituo Kidogo cha Ununuzi wa Dhahabu Mwime.
Kamishna wa Madini Mhandisi David Mulabwa ( kushoto) na Watalaam kutoka Tume ya Madini wakifuatilia jambo wakati wa kikao cha ndani baina ya ujumbe wa Wizara na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Shinyanga.
Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza jambo wakati wa kikao cha ndani kabla ya kuanza ziara. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainabu Taleck.
……………………………..
Na Asteria Muhozya, Kahama
Waziri wa Madini Doto Biteko ametoa Onyo la Mwisho la Kukifungia Kituo cha Uchenjuaji Dhahabu cha Jema Afrika kilichopo Wilayani Kahama.
Hatua hiyo inafuatia kubainika kwa jaribio la wizi wa dhahabu uliofanywa na baadhi ya wafanyakazi wa kituo hicho kutaka kuiba dhahabu ya mteja.
Akizungumzia tukio hilo, Waziri Biteko amewataka wamiliki wa kituo hicho kuandika barua ya kuweka makubaliano na Serikali ya kutojirudia tena kwa vitendo vya wizi kituoni hapo.
‘’Ni jicho la huruma tu tukiwapeleka mahakamani mali zenu zitataifishwa. Tunajua mmewekeza mitaji yenu na mna mikopo. Nilishamwambia mmiliki kuwa kituo chako kina rekodi ya wizi. Rais anawapenda, anawapigania ili watanzania wamiliki uchumi wa madini lakini mnamuangusha kwa kutofuata taratibu,’’ amesisitiza Waziri Biteko.
Amewatahadharisha wamiliki wa vituo vya uchenjuaji nchini kuhusu wizi wote wa dhahabu unaofanyika na kuwasisitiza kwamba, unafahamika na kuwataka wote wanaojihusisha na vitendo hivyo kujiepusha na kwa wale wasiotaka kufanya kazi zao kwa uaminifu watafute biashara nyingine.
Mbali na kutembelea kituo hicho, pia, Waziri Biteko na ujumbe wake wametembelea Kituo Kidogo cha Ununuzi wa dhahabu kilichopo katika eneo la Wachimbaji wadogo wa Mwime ambapo amewapongeza kwa kufuata taratibu na Sheria na kuwataka kufanya kazi zao kwa amani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Taleck amesema Mkoa huo unahitaji wawekezaji lakini walio waaminifu.Ameongeza kuwa, wizi na udanganyifu katika kiwand cha uchenjuaji Jema Afrika ulibainiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama na kutumia fursa hiyo kuwatahadharisha wote wasiofuata taratibu kuwa serikali inawaona na itawafikia.
Katika ziara hiyo, Waziri Biteko pia ameongozana na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Shinyanga, Kamishna wa Madini Mhandisi David Mulabwa na Watalaam kutoka Tume ya Madini.
Aidha, ziara hiyo imefanywa wakati ambapo wizara na wadau wengine wa madini wanashiriki Maonesho ya Pili ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini Mkoani Geita yanayotarajiwa kuhitimishwa Septemba 29, 2019.Ziara hiyo imefanyika Septemba 28, 2019
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇