Waziri Mkuu wa Zamani wa Tanzania, Edward Lowassa amesema kuwa utendaji kazi wa Rais John Pombe Magufuli wa nchi hiyo umeliwasha moto kila mahali taifa hilo.
Lowassa ameyasema hayo leo katika mahafali ya shule ya msingi ya Meyers mjini Arusha, ambapo amesema kwamba, hatua ya kuondolewa kazini kwa watendaji wazembe na wasiotimiza wajibu wao wa kazi, imeifanya nchi kushika adabu. "Rais Magufuli anastahili pongezi anafanya kazi nzuri sana, tunaona mawaziri wanafanya kazi nzuri , Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) yupo kule wengine huku, nchi imewaka moto kila sehemu.” Amesema mwanasiasa huyo aliyechuana na Rais John Pombe Magufuli kwenye uchaguzi wa rais mwaka 2015, wakati akipeperusha bendera ya upinzani nchini humo. Kwa mujibu wa Lowassa, kazi za Rais Magufuli, zinatakiwa kupakwa ‘poda’ kwa kuhusisha uboreshaji wa elimu ambayo itawapa ujuzi wahitimu kujiajiri. "Kuna vijana wengi wanamaliza masomo kutokana na mpango wa elimu bure sasa tujitahidi elimu hii iwasaidie vijana kupata ujuzi na ubunifu ili kuweza kujiajiri."
Ameongeza Lowassa. Waziri huyo mkuu wa zamani wa Tanzania alitangaza kurejea ndani ya chama tawala CCM mwanzoni mwa mwezi Machi mwaka huu. Katika radiamali yake kiongozi wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe alisema kuwa, katika dhoruba za miaka mwili ambazo alizishuhudia wakati akiwa ndani ya chama hicho Edward Lowassa, alilegea kuliko mlenda. Mbowe alibainisha kwamba, Mzee Lowassa aliyejiunga ndani ya Chadema tarehe 28 Julai 2015 na kupitishwa kuwa mgombea urais wa chama hicho akiungwa mkono na vyama rafiki vya Ukawa, alishindwa kuhimili mikikimikiki ya upinzani na kuamua kurejea ndani ya chama tawala CCM tarehe mosi Machi mwaka huu.
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇