Kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu, CHADEMA wilayani Nachingwea kimepata pigo kwa kuhamwa na aliyekuwa katibu wake wilaya, Hamisi Majaliwa, ambae ametaja sababu za kuhama chama hicho.
Akizungumza na Muungwana Blog, Majaliwa aliyejiunga na Chama Cha Mapinduzi( CCM) juzi katika tawi la Kilimanihewa na kupokelewa leo na katibu wa CCM wa mkoa wa Lindi katika ukumbi wa chuo cha walimu Nachingwea. Alisema amehama kutoka CHADEMA kutokana na kuchoshwa na mwenendo mbaya wa chama hicho.
Alisema alivumilia muda mrefu akiamini ataona mabadiliko, lakini hakuona. Badala yake ameshuhudia ukiukwaji wa katiba ya chama, taratibu na kanuni. Hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani.
Alisema kuelekea uchaguzi mkuu wa mwakani baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu ya wilaya ambao wanatamani kuwa wagombea wa ubunge kwenye majimbo wanapanga safu za viongozi wa wilaya kwa maslahi yao.
'' Umefanyika uchaguzi wa wilaya nakupata viongozi ambao walipatikana kupitia kikao kisichorasmi kilichofanyika Nangowe. Kikao ambacho kiliandaliwa na kiongozi anaetaka ateuliwe na chama kuwa mgombea wa ubunge. Sisi wajumbe wa kamati ya utendaji ambao tulionekana hatumuungi mkono hatukuwepo,'' alisema Majaliwa.
Majaliwa ambae alijinasibu kuwa alikuwa katibu wa wilaya nasio kaimu kutokana kuhudumu miaka miwili alisema hata kwenye mkutano mkuu wa wilaya wajumbe 25 wakamati ya utendaji ya wilaya hawakuhudhuria. Huku akienda mbali zaidi kwakusema '' Sisi ambao alituona hatukuwa upande wake tulinyang'anywa kadi kabla ya mkutano huo. Kwahiyo hatukuwa nasifa ya kuingia mkutanoni, mpaka sasa sikuwa na kadi ya CHADEMA,'' alidai Majaliwa.
Alisema kwakuwa hataki kuwa sehemu anguko la chama hicho wilayani humu katika chaguzi zijazo ameamua kujiweka pembeni( kujiondoa) kutoka katika chama hicho ili asibebeshwe lawama kikifanya vibaya kwenye chaguzi hizo.
Katika hali inayothibitisha hali sio shwari ndani ya chama hicho, mmoja wa viongozi wastahafu wa wilaya ambae hakutaka jina lake litajwe katika habari hii licha ya kusikitishwa na uamuzi wa Majaliwa alisema '' Tunatengeneza maadui wengi ndani ya chama badala ya kuuwa adui yetu mmoja tu CCM. Haiko sawa, na itatugharimu,'' alisema bila kufafanua kada huyo wa CHADEMA.
Juhudi za kuwapata viongozi wa wilaya wa chama hicho ili wathibitishe au kukanusha madai ya Majaliwa na kada huyo mstahafu zinaendelea.

No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇