Na Issa Mtuwa Dodoma
Kufuatia ziara aliyofanya Waziri wa Madini Doto Biteko mkoani Lindi na Mtwara hususani wilaya ya Nachingwea na kuibua sintofahamu juu ya Kampuni ya Ngwena Ltd kuhusu ushirika wake na Kampuni ya Indiana kutoka Australia, suala hilo limefanya Uongozi wa Kampuni ya Indiana kupitia Mkurugenzi wake Bob Adam kuja nchini kukutana na Waziri wa Madini ili kujadili kuhusu ushirika wao na Ngwena Ltd.
Agosti 19, 2019 Waziri Biteko amekutana na kuzungumza na mkurugenzi huyo kuhusu ushirika wao wa kuunganisha kampuni hizo bila kuijulisha wizara.
Waziri Biteko amembana mwekezaji huyo kwa hoja tatu zilizopelekea kutopatikana majibu ya moja kwa moja kutokana na kuto kuwepo kwa mwakilishi wa upande wa pili wa kampuni ya Ngwena Ltd.
Hoja hizo ambazo waziri Biteko alitaka kufahamu kutoka kwa kampuni ya Indiana ni; mosi, makubaliano kati ya Indiana na Ngwena hayana taarifa kwa Wizara, ni kwa nini waliamua kuunganisha bila kuijulisha Wizara wakati kampuni moja ni ya Kitanzania na nyingine ni ya kigeni... Mbili, Wizara inataka kuona makubaliano yao ya kimaslahi (fair deal) baina ya pande zote ili pia wizara ijue serikali inafaidikaje? Na tatu, kampuni husika zinatunzaje shehena kubwa ya sampuli za madini bila kuijulisha Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ambayo ndio yenye dhamana ya utunzaji?
Aidha, waziri Biteko aliendelea kuibana kampuni hiyo ya Indiana kupitia mkurugenzi wake huyo kwa kumuuliza uhusika wake katika kampuni ya Ngwena Ltd huku Mkurugenzi wa huduma za Sheria wa Wizara ya Madini Edwin Igenge akimhoji ni tangu lini ushirika wake na Ngwena ulianza? Je, ni kabla au baada ya marekebisho ya Sheria ya Mwaka 2017?
Akitoa majibu kwa baadhi ya hoja na maswali, Bob Adam amesema Indiana ndio inayomiliki Ngwena Ltd na kufadhili kifedha na masuala mengine. Kuhusu kabla au baada ya marekebisho ya sheria ya 2017 Adam hakuwa na uhakika wa moja kwa moja na alisema mpaka arejee kwenye nyaraka ili ajiridhshe.
“Kampuni yetu ndio inayo miliki Ngwena Ltd kwa maana Indiana inamiliki 60% ya hisa zote na ndio maana ninasema Indiana inamiliki Ngwena,” amesema Bob Adam.
Kutokana na hoja tatu za msingi kutopatiwa majibu ya kuridhisha kwa kukosekana kwa Uongozi wa Ngwena Ltd katika kikao hicho, Waziri Biteko ametaka kupangwa kwa tarehe nyingine huku akimtaka Adam kurudi tena nchini akiwa na uongozi wa Ngwena Ltd ili kufahamu kiundani juu ya makubaliano yao kwani mpaka sasa kampuni inayotambuliwa na wizara ni Ngwena Ltd na siyo Indiana.
Wiki iliyopita Waziri wa Madini alifanya ziara mkoani Lindi wilaya ya Nachingwea na kutembelea eneo la Nditi ambalo kampuni ya Ngwena Ltd imewekeza, moja ya mambo aliyokutana nayo ni uwepo wa makubaliano (Joint-Venture) kati ya kampuni ya Ngwena Ltd na Indiana kutoka Australia kinyume cha sheria na uwepo wa shehena kubwa ya sampuli za madini zilizohifadhiwa kinyume cha sheria.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇