Hayo yalizungumzwa na mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi wakati akifungua rasmi uzinduzi wa programu ya Huduma za Hali ya Hewa kwa Afrika (Weather Information and Services for Africa (WISER) Kitaifa “WISER National Project” katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam, Tanzania.
‘Programu hiyo itaiwezesha Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kusambaza taarifa za hali ya hewa pamoja na kuelimisha wadau mbalimbali juu ya matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa hususan katika sekta za Kilimo, Usafiri majini, Udhibiti wa majanga, Maji na Nishati hivyo itaongeza nguvu katika kuwafikia wananchi wengi’,alizungumza Dkt. Kijazi.
Aidha, aliendelea kueleza kuwa madhumuni makubwa ya program ya WISER Kitaifa ni kuhakikisha kunakuwa na matumizi sahihi ya tarifa za hali ya hewa katika sekta mbali mbali za maendeleo kwa lengo la kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.
Kwa upande wa mratibu wa programu ya WISER kwa Nchi za Afrika Mashariki, Ndugu. John Mungai alieleza kuwa lengo la warsha ya uzinduzi huo ni kuwakutanisha wadau na kuwa na uelewa wa pamoja wa programu hii pia kutoa taarifa ya kuanza kwa utekelezaji wake kwa wadau wanaohusika katika program hii.
Awali Rais wa TMS Dkt. Burhani Nyenzi aliwajulisha washiriki kuwa tayari utekelezaji wa awali umeanza kufanyika kwa kuwajengea uwezo wadau wa sekta husika pamoja na wanahabari katika mikoa ya Dodoma, Simiyu, Tanga na Manyara.
Programu hii inafadhiliwa na Serikali ya Uingereza kupitia Shirika lake la Kimataifa la maendeleo (DFID) na ulijumuisha wadau mbalimbali wakiwemo wizara na taasisi za serikali, taasisi zisizo za kiserikali (NGO), mashuleni, watendaji wa vijiji na wanahabari.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇