Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ametatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda wa miaka 10 kati ya wanakijiji wa Kumbulu na msitu wa Hifadhi ya Kumbulu unaosimamiwa na Halmashauri ya wilaya ya Gairo kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)
Mhe. Kanyasu amesema mgogoro huo wa ardhi ulianza mwaka 2009 baada ya kijiji hicho kupanga matumizi bora ya ardhi ambapo kutokana na baadhi ya viongozi wa kijiji hicho kutokuridhia uamuzi huo na kuanza kuwachochea wananchi kuendesha shughuli za kibinadamu ndani ya msitu huo.
Kufuatia hali hiyo, Kanyasu ameagiza kamati iliyosheheni wataalam mbalimbali ambayo ilikwisha undwa na wilaya ya Gairo igawe upya maeneo hayo kwa kuzingatia idadi ya watu katika kijiji hicho kwa kuongeza eneo la kilimo kutoka ekari 1,000 hadi ekari 2,314 kwa kulimega eneo la msitu wa hifadhi wenye ukubwa wa ekari 5,500 hadi 5000 ili eneo hilo litumike kwa ajili ya kilimo.
Aidha, Kanyasu ameagiza eneo la malisho lipunguzwe kutoka ekari 1,641 hadi ekari 1,000 ili ekari 641 iweze kutumika kwa ajili ya kilimo.
Ameyatoa maagizo hayo wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kumbulu wilayani Gairo katika mkoa wa Morogoro.
Kutokana na malalamiko hayo ya wananchi, Kanyasu aliwaeleza wananchi hao kuwa mpango wa matumizi bora ya ardhi uliofanyika mwaka 2008 ulibainika kuwa na kasoro kwa vile baadhi ya wananchi walichukua ardhi kubwa na kuna wengine walichukua na kuiuza na kuna wengine walihamia kijijini hapo kwa ajili ya kutafuta ardhi.
Akizungumzia kuhusu ugawaji huo wa ardhi kwa kila kaya, Mhe. Kanyasu amesema kijiji hicho kina kaya 642 hivyo kila kaya itagawiwa ekari mbili na hivyo kufanya jumla ya ekari 1,284 kati ya ekari 2,314.
Awali, mpango huo wa matumizi bora ya ardhi ulitenga eneo la misitu wa hifadhi ekari 5,500, eneo la kilimo ekari 1,000 pamoja na eneo la malisho la ukubwa wa ekari 1, 600 lakini bado viongozi wa kijiji hicho licha ya kushirikishwa katika mpango huo waliendelea kuwahamasisha wananchi kuvamia misitu huo kwa madai kuwa hawayatambui maamuzi hayo.
Aidha, Mhe. Kanyasu amesema kwa vile Msitu huo wa Hifadhi unapakana na vijiji vitatu ni vyema na vijiji viwili mbali na kijiji cha Kumbulu kama navyo vina uhitaji ya ardhi viwasilishe maombi yao ili kupunguza migogoro.
Katika hatua nyingine, Mhe, Kanyasu amezionya kaya hizo zitakazopata ardhi ziendeleze ardhi hiyo la sivyo zitanyang’anywa.
Pia, Kanyasu amevionya vikundi vya watu wenye maslahi binafasi ndani ya kijiji hicho viache tabia ya kuchochea migogoro ya ardhi la sivyo Serikali haitasita kuvichukulia hatua kali za kisheria.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe Amewataka wananchi hao kutoa ushirikiano kwa Kamati hiyo wakati itakapokuwa ikitekeleza majukumu yake ili kila kaya iweze kupata ardhi kwa ajili ya kilimo
‘’Lazima mpate ardhi ya kilimo lakini ni muhimu pia kutunza miti iliyopo kwa vile bila miti hakuna kilimo kwa sababu miti inasidia kuleta mvua. Alisisitiza Mchembe
Naye, Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby amewataka wananchi hao wakati wakisubili kugawiwa maeneo kwa ajili ya kilimo wajiepushe na ukataji miti ovyo katika msitu wa Hifadhi ya Kumbulu.
‘’ Kwa wale wanaotaka kukata miti kwa ajili ya kuchoma mkaa kwa ajili ya kuupeleka sokoni ni lazima mfuate sheria, hata ukitaka kuukata miti uliopo nyumbani kwako lazima uombe kibali kwa mamlaka inayohusika.’’ Alisisitiza Shabiby
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇