Mashambulizi ya ndege za kivita za Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) dhidi ya askari wa serikali iliyojiuzulu ya Yemen katika mikoa ya Aden na Abyan yamesababisha mauaji ya watu wasiopungua 40 na kujeruhi wengine zaidi ya 70.
Mapigano na vita vya niaba baina ya mamluki na vibaraka wa Saudi Arabia na Imarati vimepamba moto huko kusini mwa Yemen. Askari wa Abdrabbuh Mansur Hadi, rais aliyejiuzulu na kutorokea Saudi Arabia wa Yemen wametoa kipigo kwa wapiganaji wa Baraza la Mpito la Kusini wanaofadhiliwa na Imarati huko kusini mwa Yemen na kutwaa tena ikulu ya rais ya al Maashiq mjini Aden. Kufutia ushindi huo, ndege za kivita za Imarati zimefanya mashambulizi makali dhidi ya askari wa Mansur Hadi na kuua makumi ya watu. Waziri wa Habari wa Mansur Hadi, Muammar al-Aryani, amesema kuwa: "Mashambulizi hayo ya Imarati ni uhalifu na jinai kubwa na yanaonesha kuwa, Abu Dhabi haitaki kuona serikali ya Abdrabbuh Mansur Hadi ikidhibiti tena taasisi za serikali na hatua hiyo inapingana na malengo ya muungano wa Saudia ambao Imarati pia ni mwanachama wake."
Haya yote yanaakisi hitilafu kubwa zilizopo ndani ya muungano huo. Imarati imeamua kukabiliana na serikali iliyojiuzulu na rais wake aliyekimbilia Riyadh na inafanya jitihada za kuhakikisha kwamba, Baraza la Mpito la Kusini linadhibiti maeneo ya kusini mwa Yemen na kumtimulia mbali Mansur Hadi na serikali yake. Japokuwa Wizara ya Ulinzi ya Imarati imeyataja mashambulizi yaliyofanywa na ndege za kivita za nchi hiyo katika mikoa ya Aden na Abyan kuwa ni hatua ya kujihami mkabala wa hujuma za makundi ya kigaidi, lakini ukweli ni kwamba, Abu Dhabi inataka mamluki na vibaraka wake washike madaraka, na serikali kibaraka wa Saudia ya Mansur Hadi ivunjiliwe mbali.
Abu Dhabi ni mshirika mkubwa zaidi wa Saudi Arabia katika vita vya Yemen na sasa inataka mgao na kipande chake cha "keki" katika vita hivyo vinavyoendelea kwa kipindi cha miezi 53. Mbali na hayo, Imarati inataka kupewa udhibiti wa baadhi ya maeneo muhimu ya kusini mwa Yemen kama Bandari ya Aden. Hata hivyo Saudi Arabia haikubaliani na msimamo huo wa Imarati hasa kwa kutilia maanani kwamba, lengo kuu la vita vya Saudia dhidi ya Yemen ni kuirejesha madarakani serikali ya Abdrabbuh Mansur Hadi na kuhakikisha kwamba, harakati ya Ansarullah haishiki madaraka nchini humo.
Saudi Arabia inaona kuwa, imarati imeamua kuchukua misimamo kivyakevyake katika vita vya Yemen na suala hilo ndilo lililozidisha mgawanyiko na ufa kati ya Riyadh na Abu Dhabi. Shirika la habari la Reuters limenukuu vyombo vya kuaminika vikisema kuwa: "Kunaonekana ishara za kujitokeza mgawanyiko katika muungano wa Saudia na Imarati, na katika mazungumzo yake ya tarehe 11 Agosti huko Makka na Abdrabbuh Mansur Hadi, Mfalme Salman wa Saudia alieleza kutoridhishwa kwake na msimamo wa Imarati wa kujichukulia maamuzi kivyakevyake."
Kwa kuzingati hali hiyo inatabiriwa kwamba, mashambulizi ya anga ya Imarati dhidi ya mamluki na vibaraka wa Saudia yataendelea kushuhudiwa katika maeneo ya kusini mwa Yemen. Kwa msingi huo, ili kuzuia kushindwa kikamilifu huko Yemen, Saudi Arabia haitakuwa na njia nyingine isipokuwa ama kumuweka kando Abdrabbuh Mansur Hadi na kuchukua "mwanasesere" mwingine badala yake, au kukabiliana na mamluki wa Imarati na hata kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya waitifaki wa Abu Dhabi. Wakati huo waitifaki wakuu katika muungano wa vita dhidi ya taifa la Yemen watakuwa wameweka kando rasmi ushirika huo na kukabiliana uso kwa uso. Hii, kama wanavyosema wahanga, ndiyo hatima ya wavamizi na madhalimu wote katika historia ya binadamu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇