Taasisi mbili za kutetea haki za binadamu zimetangaza kuwa, hatua ya muungano vamizi huko Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia ya kuizingira nchi hiyo imesababisha kuaga dunia wagonjwa elfu 32 nchini humo.
Saudi Arabia ilianzisha vita vya Yemen mwezi Machi mwaka 2015 na vita hivyo vinaendelea kwa kipindi cha miezi 53. Vita hivyo vimepelekea kuuliwa na kujeruhiwa watu karibu elfu 60 ikiwa ni matokeo ya moja kwa moja ya mashambulizi ya ndege za kivita za muungano huo vamizi dhidi ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu. Mbali na kuishambulia Yeme, Saudi Arabia pia imeiwekea nchi hiyo mzingiro wa nchi kavu, anga na baharini. Kiasi kwamba hakuna misaada yoyote ya kibinadamu inayoingia huko Yemen. Hatua hiyo ya Saudia imekuwa na madhara na taathira mbaya sana kuliko vita. Kuzingirwa Yemen kumewasababisha raia wa nchi hiyo uhaba wa chakula na njaa huku milipuko ya magonjwa mbalimbali ikiikumba nchi hiyo. Taasisi za Umoja wa Mataifa zimearifu kuwa, asilimia 80 ya jamii ya watu milioni 24 wa Yemen wanakabiliwa na uhaba wa chakula na wanahitaji misaada ya kibinadamu.
Kuzingirwa pande zote nchi hiyo maskini kumekuwa kikwazo cha kuingizwa nchini humo dawa za kuwatibu wagonjwa na kumekuwa sababu ya kuenea maambukizo ya maradhi ya aina mbalimbali. Aidha mbali na Wayemeni karibu milioni 1.5 kuugua ugonjwa wa kipindupindu, raia wengine wengi wa nchi hiyo wanaosumbuliwa na maradhi makali wanakabiliwa na matatizo mbalimbali yanayotokana na uhaba wa zana za tiba na dawa na maelfu ya wengine wamepoteza maisha kwa masaibu hayo.
Wakati huo huo kuzingirwa mji mkuu wa Yemen, Sana'a, na kusimama shughuli za uwanja wa ndege wa mji huo kunawalazimisha wagonjwa wengi kusafiri msafa marefu kwa njia ya barabara na kwa taabu sana, safari ambayo huchukua hata muda wa siku nzima ili kuweza kutoka nje ya Sana'a kwa ajili ya kupata matibabu. Aghalabu ya wagonjwa hao hupoteza maisha kabla ya kupata huduma za matibabu.
Taarifa iliyotolewa na Baraza la Wakimbizi la Norway na shirika lisilo la kiserikali la Huduma ya Matunzo na Usahilishaji wa Ushirikiano imeeleza kuwa mzingiro wa anga huko Yemen unazuia kutolewa huduma za tiba kwa wagonjwa na tangu uwanja wa ndege wa Sana'a ufungwe Agosti 8 mwaka 2016 hadi hivi sasa raia wa Yemen karibu elfu 32 wameaga dunia kutokana na kushindwa kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Tunaweza kusema kuwa ingawa mzingiro huo uliwekwa kutokana na vita vilivyoanzishwa na Saudi Arabia huko Yemen na unahesabiwa kuwa sehemu ya vita hivyo, lakini madhara na taathira za kibinadamu za mzingiro huo ni kubwa sana kulinganisha na mashambulizi yanayofanyika dhidi ya nchi hiyo. Muhammad Abdi Mkurugenzi wa Baraza la Wakimbizi la Norway amesema kuhusu suala hilo kuwa: "Kufungwa uwanja wa ndege wa Sana'a kumesababisha kuaga dunia maelfu ya Wayemeni. Inaonekana kuwa mauaji ya Wayemeni yaliyosababishwa na makombora, mabomu na gesi za chlorine hayatoshi kwa muungano wa vita wa Saudia." Muhammad Abdi ameongeza kuwa, hakuna kisingizio chochote za kuzuia kupelekwa wagonjwa wa Yemen nje ya nchi kwa ajili ya matibabu ili kunusuru maisha yao.
Nukta ya mwisho ni kuwa, stratejia kama hii ya mzingiro inatekelezwa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Ghaza tangu mwaka 2006 dhidi ya watu wa Palestina na Ghaza ikigeuka na kuwa jela kubwa zaidi ya wazi duniani. Maumivu ya pamoja ya Ghaza na Yemen ni kwamba, mbali na pande mbili hizo kusumbuliwa na hali mbaya zaidi ya kibinadamu duniani, vilevile zimepuuzwa na taasisi za kimataifa. Hii ni kwa sababu nchi zinazodai kutetea haki za binadamu ndizo zinazounga mkono jinai hizo za Israel na Saudia dhidi ya watu wa Yemen na Palestina.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇