Waziri Mkuu wa Iraq Adil Abdul-Mahdi ametoa amri ya kuundwa kamati ya uchunguzi kwa ajili ya kuchunguza shambulio la anga lililotekelezwa katika kambi ya Harakati ya Hashdu sh-Sha'abi katika jimbo la Salah ad Din.
Hatua hiyo imekuja baada ya kambi ya harakati hiyo ya wananchi katika eneo la Amerli, mashariki mwa jimbo hilo kushambuliwa. Kwa mujibu wa habari hiyo, Adil Abdul-Mahdi, Waziri Mkuu wa Iraq ametoa amri ya kuundwa kamati maalumu ya uchunguzi kutoka makao makuu ya jeshi, kitengo cha operesheni maalumu, kikosi cha anga na kamati za wananchi. Hii ni katika hali ambayo kitengo cha uenezi wa usalama nchini Iraq, kimetangaza kwamba katika hujuma dhidi ya kambi hiyo ya Harakati ya Wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi mtu mmoja aliuawa na wengine wawili walijeruhiwa. Baadhi ya duru za habari nchini Iraq pia zimetangaza kuwa shambulizi hilo lilifanywa na ndege isiyo na rubani ya utawala haramu wa Kizayuni Israel, huku zingine zikisema kuwa lilifanywa na ndege ya Kimarekani.
Hadi sasa bado taarifa kamili kuhusiana na hujuma hiyo haijawekwa wazi. Harakati ya Hashdu sh-Sha'abi iliundwa mwaka 2014, kupitia fatwa ya kiongozi mkuu wa kidini nchini Iraq Ayatullah Sayyid Ali Sistani, baada ya kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) kuvamia na kuyakalia kwa mabavu maeneo na miji kadhaa ya Iraq. Kufuatia juhudi kubwa za kimapambano hatimaye ilifanikiwa kulisambaratisha kundi hilo la kigaidi, ambapo mwaka 2016 bunge la Iraq liliiweka Hashdu sh-Sha'abi chini ya usimamizi wa amiri jeshi mkuu wa nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇