Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Alexander Mrosso akimpima mtoto kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography) wakati wa maonyesho ya 43 ya biashara ya kimataifa yanayofanyika jijini Dar es Salaam. Katika maonyesho hayo Taasisi hiyo inatoa huduma za ushauri, vipimo na tiba za magonjwa ya moyo bila malipo kwa wananchi wanaotembelea banda hilo lililopo Banda la Jakaya Kikwete.
(PICHA NA JKCI)
Na Mwandishi Maalum
12/7/2019 Wananchi 1776 wamepata huduma za ushauri, vipimo na tiba za magonjwa
ya moyo bila malipo zinazotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
kwenye maonesho ya 43 ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam yanayofanyika
katika uwanja wa Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere uliopo barabara ya Kilwa.
Wananchi hao waliotembelea banda la Taasisi hiyo kwa ajili ya kupima afya zao walifanyiwa vipimo vya magonjwa ya moyo ambapo 448 walifanyiwa kipimo cha kuangalia jinsi
moyo unavyofanya kazi (Echocardiography), na 1097 walifanyiwa kipimo
cha kuangalia umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiogram - ECG).
Asilimia 60 ya watu waliofanyiwa vipimo walikutwa
na uzito mkubwa, asilimia 40 walikutwa
na tatizo la shinikizo la juu la damu na
asilimia 20 walikutwa na tatizo la kuwa
na sukari kwenye damu.
Aidha Taasisi hiyo hadi sasa imetoa rufaa ya
moja kwa moja kwa watu 73 wakiwemo
watoto 2 ambao baada ya kuwafanyia vipimo walikutwa na matatizo ya moyo
yanayohitaji kufanyiwa uchunguzi wa kina na matibabu ya kibingwa .
Akizungumzia mara baada ya kupata huduma ya
matibabu katika banda hilo mkazi wa Shekilango jijini Dar es Salaam Rehema
Abdalah aliipongeza Taasisi hiyo kwa
kutoa huduma ya matibabu ya moyo kwa wananchi bila malipo pamoja na kuwapa
kipaumbele wazee waliojitokeza kwenda kupima afya zao.
“Nawashukuru wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete wanaotoa huduma katika maonesho haya, kutokana na umri wangu
wamenipa kipaumbele cha kufanyiwa vipimo kwa haraka. Nimekutwa na tatizo la shinikizo
la juu la damu na tayari nimepatiwa dawa kwa ajili ya matibabu,” alishukuru Rehema.
Naye mkazi wa Mwananyamala jijini Dar es
Salaam Hatibu Rashid ameishukuru Taasisi hiyo kwa kuwafikiria wananchi wenye
uwezo wa chini kupata nafasi ya kufanyiwa vipimo vya magonjwa ya moyo na
wafanyakazi wa Taasisi hiyo pindi
watakapopata nafasi watoe huduma kama hiyo kwa wananchi waliopo maeneo mbalimbali hapa
nchini hasa vijijini.
Rashid alisema, “Zamani vipimo kama hivi
vilikuwa vinafanyika nje ya nchi tena kwa watu wenye hela. Lakini leo hii
vipimo hivi vinafanyika hapa nchini na tunafanyiwa wananchi wa kawaida kabisa.
Ninaishukuru sana Serikali kwa kuimarisha huduma ya matibabu ya moyo na
ninawaomba wananchi wenzangu watumie maonesho haya kufika katika banda la
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa ajili ya kupima afya zao bila malipo”,.
Katika maonesho hayo Taasisi hiyo inatoa bila
malipo huduma za ushauri wa lishe bora kwa afya ya moyo, umuhimu wa kufanya
mazoezi, vipimo na tiba za magonjwa ya moyo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇