Rais Donald Trump wa Marekani ambaye baada ya nchi yake kujiondoa kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA alitaka kufanyika mazungumzo mapya na Iran, ingawa hakupata jibu chanya kutoka kwa Tehran, sasa amesema kuwa kufikiwa makubaliano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni suala gumu sana.
Trump aliyasema hayo jana katika ikulu ya White House wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mzozo wa hivi karibunbi kati ya nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza: "Hao Wairani, hawatuheshimu, na kutaka nifikie makubaliano nao katika mazingira ya sasa, ni jambo zito sana kwangu." Rais huyo wa Marekani ambaye anakosolewa sana kutokana na kufeli siasa zake zinazoitwa, 'mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran' amedai kwamba, 'Huenda Washington ikajiandaa kwa ajili ya senario mbaya zaidi kuhusiana na Iran.' Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Trump ametoa radiamali kufuatia kutiwa mbaroni majasusi kadhaa wa nchi hiyo na Wizara ya Intelejensia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema kuwa: "Wairani wanasema uongo."
Hii ni katika hali ambayo Jumapili iliyopita Wizara ya Intelejensia ya Iran ilitangaza habari ya kusambaratisha mtandao wa kijasusi wa Shirika la Kijasusi la Marekani CIA nchini hapa. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, jumla ya watu 17 wenye uzoefu wa Shirika la Kijasusi la nchi hiyo CIA ambao walikuwa wakiendesha shughuli zao kwa namna ya kikundi na mtu mmoja mmoja ndani ya Iran, walitiwa mbaroni mwaka jana wa Kiirani. Aidha Wizara ya Intelejensia ya Iran ilisema kuwa majasusi hao walikuwa wakijishughulisha katika maeneo muhimu kama vile sekta za uchumi, nyuklia, miundombinu na jeshini.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇