LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 12, 2019

SERIKALI YAKAGUA UTAYARI WA MKOA WA KIGOMA

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile leo ametembelea baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Kigoma kuona utayari wa mkoa huo katika kukabiliana na ugonjwa wa Ebola.

Dkt. Ndugulile ametembelea maeneo ya Bandari kuu ya Mkoa, Uwanja wa ndege, bandari ndogo ya Kibirizi na Zahanati ya Bangwe ambayo imetengwa maalumu kwa ajili ya kutoa matibabu kwa mtu atakayebainika kuwa na virusi vya Ebola.

Naibu Waziri ameonekana kutoridhishwa na utayari wa Mkoa katika kukabiliana na ugonjwa wa Ebola nchini huku akiitaka timu iliyoandaliwa chini ya Mkuu wa Wilaya Samson Anga na Mganga Mkuu wa Mkoa Paul Chaote kuendelea kutoa mafunzo kwa timu iliyoandaliwa jinsi ya kujikinga na kutoa huduma kwa mgonjwa atakayebainika.

“Hatuna mgonjwa wa Ebola ndani ya nchi, lakini kutokana na hali ya ugonjwa huu katika nchi jirani kuna umuhimu wa sisi kama nchi kuendelea kujipanga na kuhakikisha kwamba mifumo yetu yote imekaa vizuri kipindi mgonjwa atakapojitokeza, hivyo nakuomba Mkuu wa Wilaya na Mganga Mkuu wa mkoa kuendelea kusimamia hili”. Amesema Dkt. Ndugulile.

Mapungufu aliyobaini Dkt. Ndugulile ni pamoja na wahudumu kutozingatia kanuni walizofunzwa juu ya kujikinga na maambukizi pindi watakapokua wakihudumia mgonjwa, kutokua na vifaa vya kutosha kwa ajili ya wagonjwa wa Ebola kama vitanda kwenye vituo vya Isolation na watumishi kutokua na uelewa na utayari wa kutosha kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huu.

Dkt. Ndugulile yupo Mkoani Kigoma kwa ziara ya siku tatu ambapo pamoja na maeneo mengine atatembelea mpaka wa Manyovu ili kuona hali ya utayari ya mpaka huo kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa Ebola na kisha atatembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages