LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 13, 2019

UCHUMI WETU ULIPANDA NA KUFIKIA ASILIMIA 7.0 MWAKA JANA

Serikali ya Tanzania imesema kuwa uchumi wa nchi hiyo ulikuwa na kufikia asilimia 7.0 mwaka jana ukilinganishwa na wa asilimia 6.8 mwaka 2017.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango wakati akiwasilisha bungeni jijini Dodoma taarifa ya hali ya uchumi wa nchi hiyo kwa  mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2019/2020. Akitaja sababu zilizochangia kukua uchumi wa nchi hiyo, Mpango amesema kuwa ni kupanda kiwango cha uwekezaji hususan katika miundombinu kama vile ujenzi wa barabara, reli na viwanja vya ndege.
Aidha Waziri huyo wa Fedha na Mipango ameelezea kuimarika kwa thamani ya Shilingi ya Tanzania mkabala wa sarafu ya Dola ya Marekani na kuongeza kwamba, katika kipindi kilichoishia mwezi Aprili mwaka huu, Dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa Shilingi 2,300.9 ikilinganishwa na Shilingi 2,270.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2018.
Dk Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania
Kwa mujibu wa Mpango, utulivu huo wa sarafu ya shilingi umetokana na utekelezaji wa sera ya fedha, usimamizi madhubuti wa mapato na matumizi ya serikali, matumizi ya gesi asilia badala ya kutumia mafuta na kuzalisha umeme.
Taarifa ya Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania juu ya kukua uchumi wa nchi hiyo imekuja katika hali ambayo mwezi Aprili mwaka huu Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) ulitahadharisha kuwa, uchumi wa Tanzania utadhoofika iwapo sera za sasa na sheria mpya zitaendelea kutekelezwa na serikali ya Dar es Salaam. Kwa mujibu wa mfuko huo wa Fedha IMF, uchumi wa Tanzania unakabiliwa na hali ya mdororo kwa kile ilichosema kuwa ni sera mbovu za serikali.
Hata hivyo siku chache baadaye serikali ya Tanzania kupitia Waziri huyo wa Fedha iliwataka Watanzania kutozingatia ripoti hiyo ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa madai kwamba haikuwa sahihi.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages