Ripoti mpya ya Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI) imefichua kuwa, utawala haramu wa Israel unamiliki takriban vichwa 100 vya silaha za nyuklia.
Ripoti ya taasisi hiyo iliyotolewa leo Jumatatu imebainisha kuwa, Tel Aviv inamiliki mabomu 30 aina ya gravity (yasiyo ya kuelekezwa) yanayoaminika kuundwa kwa ajili ya kuvurumisha silaha za nyuklia.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo mpya ya SIPRI, utawala wa Kizayuni wa Israel ambao ndiye mmiliki pekee wa silaha za nyuklia katika eneo la Asia Magharibi, unamiliki vichwa 50 vya silaha za nyuklia, ambavyo vinaweza kufyatuliwa kwa kombora la balestiki la ardhini. Moja ya vichwa hivyo ni kile cha Jericho III ambacho kina uwezo wa kwenda umbali wa kilomita 5,500.
Mwaka jana, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilifichua kuwa, kuna vichwa zaidi ya 80 vya nyuklia katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) na hakuna hata kimoja kati ya vichwa hivyo vya nyuklia kilichoko ndani ya ardhi ya Iran.
Kwa sasa Marekani, Russia, Uingereza, Ufaransa, China, India, Pakistan, Korea Kaskazini na utawala wa Kizayuni wa Israel ndizo zenye kumiliki silaha za nyuklia ambapo mpaka kufikia sasa, zinamiliki zaidi ya vichwa 14,000 vya nyuklia.
Utawala wa Kizayuni wa Israel unaoendesha shughuli zake za nyuklia kwa kificho huku ukiungwa mkono na Marekani hauko tayari kujiunga na Mkataba wa NPT unaopiga marufuku uundaji na uenezaji silaha za nyuklia.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇