Rais Dkt. John Magufuli
amewapongeza Watanzania kwa kuitikia mwito wa Serikali wa kuacha kutumia mifuko
ya plastiki ambayo ina madhara makubwa katika mazingira na viumbe hai wakiwemo
binadamu.
Dkt. Magufuli ametoa pongezi
hizo leo tarehe 03 Juni, 2019 wakati akizungumza na wafanyabiashara wa soko la
samaki la Feri Jijini Dar es Salaam baada ya kufanya ziara ya kushtukiza sokoni
hapo na kujionea wafanyabiashara na wanunuzi wa samaki wakitumia mifuko
mbadala.
Amempongeza Makamu wa Rais Samia
Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January Makamba, Wakuu wa Mikoa na Wakuu
wa Wilaya wote ambao wamesimamia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa tangu
mwaka 2016 kuhusu kuondoa matumizi ya mifuko ya plastiki kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, amewataka
wafanyabiashara kutotumia mwanya huo kuuza mifuko na vifungashio mbadala kwa bei kubwa na badala yake amewataka
wafanyabiashara hao pamoja na wawekezaji wa ndani na nje kujenga viwanda vya
kutengeneza mifuko na vifungashio kwa kutumia malighafi zinazopatikana hapa
nchini.
Ametoa wito kwa wananchi
kujenga utamaduni wa kuwa na vifaa vya kubebea bidhaa wanazozinunua madukani na
masokoni ili kuepuka gharama kununua vifungashio ama mifuko mbadala.
Pia Rais Magufuli ameziagiza
mamlaka zinazohusika, kuhamasisha utengenezaji wa mifuko na vifungashio mbadala
hapahapa nchini ili kuongeza ajira katika viwanda vya kutengenezea bidhaa hizo
badala ya kuacha wafanyabiashara wakigeuza nchi kuwa mahali pakuingiza bidhaa
hizo kutoka nje ya nchi.
Akiwa katika soko hilo la Feri,
Rais Magufuli amenunua samaki kutoka kwa wafanyabiashara wadogo wanaotumia
vitambulisho vya wajasiriamali na amewapongeza kwa juhudi zao za kujitafutia
kipato halali.
Ameiagiza Manispaa ya Kinondoni
kupunguza tozo ya pango kwa wapaa samaki
kutoka shilingi 1,000 hadi shilingi 500 kwa siku na ameitaka manispaa hiyo
kutenga shilingi Milioni 10 kutoka kwenye makusanyo ya soko hilo kujenga jengo
jingine la wafanyabiashara wasiouza samaki kama vile Mama Lishe, Baba Lishe na
wauza bidhaa zingine ambao hawanufaiki na jengo la wauza samaki ambalo mwaka
jana alichangia shilingi Milioni 20.
Rais Magufuli amekagua
maendeleo ya ujenzi wa jengo la wauza samaki ambalo alilichangia shilingi
Milioni 20 mwaka jana ambapo ameagiza Manispaa ya Ilala ifanye ukaguzi wa
gharama zilizotumika kutokana na kuwepo wasiwasi wa matumizi mabaya ya fedha.
Ameiagiza Manispaa ya Ilala na
Menejimenti ya soko la Feri kuweka utaratibu wa kuwapokea wafanyabiashara
wanaoingiza samaki sokoni hapo kwa muda wote wa saa 24, kuweka umeme na maji
katika jengo mojawapo la wafanyabiashara wa samaki ndani ya siku 5 na kuingiza
umeme katika jengo la huduma ya Msalaba Mwekundu (Red Cross) lililopo sokoni hapo.
Huku wakimshangilia
Wafanyabiashara wa soko la Feri wamemshukuru Dkt. Magufuli kwa jinsi
anavyowapigania Watanzania wanyonge wakiwemo wafanyabiashara wadogo na
wamemhakikishia kuwa watatekeleza maagizo yake ya kutotumia mifuko ya plastiki
kama inavyoelekezwa katika sheria ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 na
kanuni zake.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇