Rais Dkt. John Magufuli
amempongeza Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi kwa juhudi zake za kutafuta amani
nchini mwake baada ya kuingia madarakani katika uchaguzi wa kidemokrasia na kubadilishana
madaraka kwa amani uliofanyika kwa mara ya kwanza tangu nchi hiyo ipate uhuru
mwaka 1960.
Rais Magufuli ametoa pongezi
hizo leo tarehe 13 Juni, 2019 wakati akitoa hotuba katika Dhifa ya Kitaifa aliyoiandaa
kwa heshima ya Rais Tshisekedi ambaye amewasili hapa nchini leo kwa Ziara ya
Kitaifa ya siku 2 kwa mwaliko wa Rais Magufuli.
Rais Magufuli amempongeza, Rais
Tshisekedi kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa DRC katika uchaguzi wa kihistoria
uliofanyika Januari 2019 na kwa juhudi zake za kuunganisha makundi yaliyokuwa
yakipingana nchini DRC. Amemhakikishia kuwa Tanzania inaunga mkono juhudi hizo.
“Pamoja na kukupongeza wewe Rais
Tshisekedi pia nampongeza Rais Mstaafu wa DRC Joseph Kabila kwa kufanikisha
mchakato wa kubadilishana madaraka kwa amani” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amesema kwa
kutambua umuhimu wa uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo, Tanzania imekuwa
ikipokea wakimbizi wengi wanaotokana na machafuko kutoka nchini DRC na amemhakikishia
kuwa Tanzania itadumisha udugu, urafiki na ujirani mwema na nchi hiyo.
Pia amesisitiza kuwa Tanzania haitowaondoa
askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wanaoshiriki katika
operesheni ya ulinzi wa amani mpaka hapo hali ya amani itakapotengemaa.
Kwa upande wake Rais Tshisekedi
amemshukuru Rais Magufuli na Watanzania wote kwa kuendelea kuwa majirani wema
na ndugu wa kweli wa DRC na amemhakikishia kuwa Serikali yake itaimarisha
uhusiano huo ikiwemo kutilia mkazo maombi ya nchi hiyo kujiunga na Jumuiya ya
Afrika Mashariki.
Tshisekedi amebainisha kuwa
baada ya kuimarisha amani nchini DRC, Serikali yake sasa inaelekeza jitihada
katika kuimarisha usalama nchini humo na ameishukuru Tanzania kwa mchango wake
mkubwa katika ulinzi wa amani ya DRC.
“Ziara hii ni ishara ya
kuonesha kuwa DRC inatambua umuhimu wa uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania,
na sisi DRC tumejipanga kuhakikisha uhusiano huu tunaukuza zaidi” amesema Rais
Tshisekedi.
Ameongeza kuwa nchi za Afrika
zinayo changamoto ya kuimarisha utengamano wake wa kiuchumi, na kwa maana hiyo
anaona umuhimu mkubwa wa kutumia fursa mbalimbali zilizopo likiwemo Ziwa
Tanganyika katika kukuza biashara na pia kuimarisha miundombinu ya barabara,
nishati na kuondoa vikwazo vya kibiashara ili kuleta matokeo makubwa katika
siku za mbeleni.
Dhifa ya Kitaifa iliyofanyika
leo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Alhaji
Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Zanzibar Amani Abeid Karume, Waziri Mkuu
Mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba, Waziri Mkuu Mstaafu Edward Ngoyai Lowassa,
Mawaziri, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wabunge, Mabalozi na
Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Vyama vya
Siasa na wafanyabiashara.
Rais Tshisekedi kesho
asubuhi atatembelea Bandari ya Dar es Salaam ambayo hutumiwa kupitisha mizigo
ya DRC na baadaye atafanya mazungumzo rasmi na mwenyekiti wake Mhe. Rais
Magufuli kabla ya kurejea nchini DRC.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇