Rais Dkt. John Magufuli
amewataka Mawaziri na Wataalamu wa Tanzania na wenzao wa DRC (watakaoteuliwa) ndani ya mwaka huu,
kuitisha kikao cha Kamati ya Pamoja ya Ushirikiano (Joint Permanent Commission – JPC) ambacho hakijawahi kufanyika
tangu mwaka 2002 ili kujadili na kurejesha maeneo muhimu ya ushirikiano ikiwemo
ushirikiano katika usafiri wa anga kati ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) na Shirika la Ndege la Congo (Congo Airways).
Ametoa agizo hilo wakati
akimuaga mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Felix Tshisekedi ambaye amemaliza
Ziara ya Kitaifa ya siku 2 aliyoifanya hapa nchini kwa mwaliko wa Rais Dkt.
John Magufuli.
Tshisekedi ameagwa na Rais
Magufuli katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es
Salaam na kuelekea nchini Burundi.
Rais Magufuli amemtakia heri Rais
Tshisekedi katika uongozi wake na amemshauri kusimama kidete kutatua matatizo
ya wananchi wa DRC huku akisisitiza kuwa kwa utajiri wa DRC, uchumi wa nchi
hiyo haupaswi kukua kwa kiwango kidogo cha asilimia 4.
Kwa upande wake, Rais
Tshisekedi amemshukuru Rais Magufuli kwa kumwalika kufanya Ziara ya Kitaifa
hapa nchini na amebainisha kuwa lengo la ziara yake ni kuimarisha na kukuza
zaidi udugu, urafiki na uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na DRC.
Tshisekedi amesema katika
mazungumzo yake na Rais Magufuli wamekubaliana kuwa bila amani jitihada za
maendeleo katika eneo lote la maziwa makuu hazitafanikiwa, hivyo wana kila
sababu ya kuhakikisha kunakuwa na amani ya kudumu pamoja na kutumia vizuri fursa
mbalimbali za kukuza uchumi ukiwemo ukanda wa ziwa Tanganyika wenye urefu wa
kilometa 554.
Amesema ana matumaini kuwa JPC
itakayofanyika itatatua changamoto zote za kukuza biashara na uwekezaji kati ya
Tanzania na DRC na ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na Rais
Magufuli.
Pamoja na kumshukuru Rais
Magufuli kwa ahadi yake ya kuunga mkono ombi la DRC kujiunga katika Jumuiya ya
Afrika Mashariki, Rais Tshisekedi ameahidi kuhudhuria Mkutano wa 39 Jumuiya ya
Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)
utakaofanyika mwezi Agosti mwaka huu hapa Tanzania na amebainisha kuwa anaamini
kuwa SADC ni jumuiya yenye fursa na manufaa makubwa ya
kiuchumi.
Mapema leo asubuhi Rais Tshisekedi
ametembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge Railway) katika eneo la
Vingunguti Jijini Dar es Salaam na baadaye akatembelea Bandari ya Dar es Salaam
ambayo hutumika kupitisha mizigo ya DRC.
Akiwa Ikulu Jijini Dar es
Salaam Rais Tshisekedi amefanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Magufuli na
baadaye viongozi hao wamezungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari.
Rais Magufuli amemshukuru Rais
Tshisekedi kwa kufanya Ziara ya Kitaifa hapa nchini na kwa dhamira yake ya
kukuza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya DRC na Tanzania
hususani katika uchumi.
Rais Magufuli amesema kiwango
cha biashara kinachofanywa kati ya Tanzania na DRC ni kidogo ikilinganishwa na
ukubwa wa uhusiano na fursa zilizopo kati ya nchi hizo, ambapo katika mwaka
uliopita biashara kati ya Tanzania na DRC ilikuwa na thamani ya shilingi
Bilioni 305.375, wafanyabiashara wa DRC walikuwa wamewekeza nchini Tanzania
miradi 8 yenye thamani ya shilingi Bilioni 13.144 na kukiwa na Watanzania
wachache ambao wameweka nchini DRC.
Amefafanua kuwa japo kuwa sekta
ya usafirishaji inaridhisha kidogo kwa DRC kuongeza mizigo inayopita Bandari ya
Dar es Salaam kutoka tani Milioni 1.176 ya mwaka 2017 hadi kufikia tani Milioni
1.78 ya mwaka 2018, kuna haja ya kuchukua hatua madhubuti zaidi za kukuza
biashara na uwekezaji ikiwemo kuondoa vikwazo, kutumia fursa mbalimbali
zilizopo ikiwemo madini, uvuvi, kilimo, ujenzi wa viwanda na kulitumia ipasavyo
soko la nchi hizo lenye jumla ya watu Milioni 140.
Kwa upande wa Tanzania, Rais
Magufuli amesema pamoja na kujenga reli ya kati (SGR), kupanua Bandari ya Dar es Salaam, kuanzisha huduma za pamoja
za bandari kwa saa 24 (siku zote 7 za
wiki) na kuimarisha miundombinu ya barabara katika njia 8 za kuingia na
kutoka DRC, Tanzania imeongeza muda wa kusubiri bandarini kutoka siku 24 hadi
30 kwa mizigo ya DRC, imeondoa katazo la ufunguaji makontena na kufuta tozo ya
kusindikiza mizigo hadi mpakani mwa Tanzania na DRC.
Aidha, Rais Magufuli amesema
Tanzania itaikarabati meli ya MV. Liemba inayotoa huduma kati ya Tanzania (Kigoma) na DRC, itajenga meli mpya mbili
ambapo moja itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 600 na mizigo tani 400 na ya pili
itakuwa meli ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 2,000 na ameafiki mapendekezo
ya Rais Tshisekedi ya reli ya kati ya Tanzania kujengwa kutoka Isaka – Rusumo –
Kigali hadi Mashariki ya Kongo ili kufikisha mizigo moja kwa moja nchini DRC.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇