Idara Kuu ya Takwimu ya Palestina imechapisha ripoti kwa mnasaba wa mwaka wa 71 wa ardhi za Palestina kukaliwa kwa mabavu na utawala bandia wa Israel na kusema: "Idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi katika kipindi cha miaka 71 ni takribani 100,000."
Aidha taarifa hiyo imesema tokea mwaka 1967 hadi sasa, utawala wa Kizayuni wa Israel umewakamata Wapalestina takribani milioni moja.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, hivi sasa kuna Wapalestina 5700 wanaoshikiliwa mateka katika jela za utawala wa Kizayuni wa Israel ambapo 250 miongoni mwao ni watoto na 47 ni wanawake.
Hali kadhalika ripoti hiyo inasema mwaka 2018, takribani Wapalestina 6500, wakiwemo watoto zaidi ya 1000 na wanawake 140 walikamatwa na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni.
Aidha wakati wa maafa ya Wazayuni kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina miaka 71 iliyopita, karibu Wapalestina 800,000 kati ya milioni moja na laki nne walilazimika kukimbia makazi yao ya jadi.
Wapalestina hao ambao wengi walilazimika kukimbilia hifadhi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Ukanda wa Ghaza na nchi za Kiarabu walikuwa wakiishi katika ardhi zao zilizoghusubiwa ambazo leo zimepachikwa jina bandia la Israel.
Kila mwaka tarehe 15 Mei, Wapalestina hujumuika kukumbuka siku kama hii mwaka 1948 wakati ambao utawala bandia wa Israel uliasisiwa.
Siku hii ni maarufu kama Siku ya Nakba yaani maafa na katika siku kama hii, Wazayuni kwa himaya na njama za Uingiereza, walikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇