Jeshi la Marekani limetuma meli zake za kivita ambazo zimefika karibu na visiwa vya China katika Bahari ya Kusini ya China katika hatua ambayo imewakasirisha wakuu wa Beijing na hivyo kupelekea hali ya taharuki kuendelea baina ya nchi hizo mbili ambazo tayari ziko katika vita vya kibiashara.
Msemaji wa Jeshi la Marekani Clay Doss amethibitisha kuwa meli za kivita za Marekani zimepita karibu na visiwa vya China Jumatatu hii.
Eneo hilo muhimu la bahari limekuwa chimbuko la mvutano mkubwa kati ya Marekani na China kutokana na kuwa linazozaniwa na mataifa sita ya kusini mwa Asia. Marekani imekuwa ikizichochea nchi zinazodai umiliki wa eneo hilo la bahari ambalo China inasisitiza ni milki yake.
Marekani imeikasirisha China kwa kuendeleza doria ya meli na ndege zake za kivita karibu na visiwa vya Spratly vinavyomilikiwa na China.
Hayo yanajiri huku vita vya kibiashara baina ya China na Marekani vikiwa vimeshika kasi. Katika hatua ya hivi karibuni kabisa, Shirika la Google la Marekani limepiga marufuku kampuni ya simu ya pili kubwa duniani, Huawei, kutumia baadhi ya huduma zake za mfumo wa Android, hatua ambayo ni pigo kubwa kwa kampuni hiyo ya China.
Aina mpya za simu za Huawei hazitoweza kutumia baadhi ya programu tumishi kutoka Google apps.
China na Marekani, ambazo zinaongoza katika biashara duniani, zimekuwa zikizozana kwa mwaka mmoja uliopita huku mzozo huo ukiendelea kuwa mbaya kila siku.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇