Maelfu ya Wasudan jana kwa siku ya pili mfululizo wameendeleza maandamano yao nje ya nyumba ya Rais Omar al Bashir wa nchi hiyo katika eneo la kati mwa Sudan.
Maafisa wa usalama wamejaribu kuwatimua waandamanaji hao kutoka eneo hilo kwa kutumia gesi ya kutoa machozi lakini wameshindwa kusitisha vuguvugu hilo la wananchi wanaomtaka al Bashir ang'atuke baada ya kuitawala nchi hiyo kwa muda wa miaka 30.
Washiriki wa maandamano hayo ya amani nchini Sudan wanaonekana kupata motisha kufuatia mafanikio ya maandamano ya Waalegeria ambao wameweza kumalzimu rais wa nchi hiyo Abdelaziz Boutefklia ajiuzulu baada ya kuitawala nchi hiyo kwa muda wa miaka 20.
Waandamanaji wamelitaka jeshi, ambalo linalinda nyumba hiyo, kujiunga na wananchi ili kumlazimu al Bashir aondoke madarakani. Waandamanaji pia leo wamekusanyika katika mtaa wa Burri mjini Khartoum ambapo wamefunga barabara kadhaa.
Kwingineko mtu moja amepoteza maisha Jumamosi katika maandamano yaliyokuwa yakifanyika katika mji wa Omdurman ulio karibu na mji mkuu Khartoum.
Hayo yanajiri wakati ambao Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Physicians for Human Rights limesema kuwa, watu wasiopungua 60 wameuliwa na maafisa usalama nchini Sudan katika kipindi cha miezi mitatu ya ghasia na maandamano dhidi ya utawala wa kiimla wa al-Bashir.
Sudan imekumbwa na maandamano ya kumtaka Rais Omar al-Bashir aachie ngazi tangu katikati ya mwezi Disemba mwaka jana 2018, ambayo chanzo chake kilikuwa ni maandamano hayo kilikuwa ni kulalamikia kupanda bei za bidhaa muhimu hasa mkate na mafuta.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇