LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 9, 2019

HOTUBA YA MWENYEKITI WA WAZAZI TAIFA KWENYE KILELE CHA WIKI YA WAZAZI KITAIFA TAREHE 06/04/2019 MKOANI RUKWA

HOTUBA YA MWENYEKITI WA WAZAZI TAIFA KWENYE KILELE CHA WIKI YA WAZAZI KITAIFA TAREHE 06/04/2019
MKOANI RUKWA
HISTORIA YA JUMUIYA:
Jumuiya ya Wazazi ilianzishwa mwaka 1955 mwaka mmoja baada ya kuanzishwa kwa Chama Cha TANU mwaka 1954.  Hii ni baada ya Wakoloni kuilazimisha TANU  kuchagua moja, aidha kuendesha shule au kuendelea na siasa.  Mara baada ya zoezi hili Wajumbe wa TANU walitembea Majimbo yote na Mikoa ya Tanganyika kwa lengo la kuhamasisha na hivyo kupelekea kuundwa kwa vikundi mbalimbali vya Wazazi ambavyo vilichochea moto wa siasa nchini.  Miongoni mwa vikundi hivyo ni (i)   DAPA na MAPA vilivyokuwa Dar Es Salaam.

(ii)  Kikundi cha APA Mkoa wa Tanga.

(iii) Kikundi cha KANYIGO Western Lake Mkoa wa Kagera.

(iv) Kikundi cha TWIBOKE kilichokuwa Mkoa wa Mara.

Baadae vikundi hivyo vikaunganishwa tarehe 06/04/1957 na kuwa Chama kimoja kilichojulikana kwa kifupi TAPA.  Chama hicho kiliandikishwa rasmi katika daftari la Serikali ya Kikoloni kwa namba 1237, kwa sababu ya hoja hii ndiyo maana leo Umoja wa Wazazi wanasherehekea siku ya Wazazi kila ifikapo tarehe 06/04


ya kila mwaka.  Na kwa msingi huo TAPA ilikuwa chombo cha kwanza cha TANU kufanya kazi ya siasa na Elimu.

Lengo kuu la kuanzishwa kwa Jumuiya hii ilikuwa ni kusimamia na kutoa elimu kwa Watanganyika, Jumuiya ilikabidhiwa jumla ya shule za msingi 233 zilizokuwa na takribani wanafunzi 15,000.  Kwa nchi nzima.

Jumuiya ilikabidhiwa jukumu la kuendesha shule kutokana na ukandamizaji wa Wakoloni dhidi ya Chama Cha  TAWA, Kilichokuwa kinafanya kazi ya siasa na hivyo utawala wa Kikoloni ukaona TANU itaziendesha shule na Taasisi za Elimu basi hali yao ingekuwa mbaya. Hivyo TAPA kupewa jukumu la kusimamia Elimu na Malezi kwa jamii na watoto wa Kitanzania.

Mara baada ya Uhuru na mpaka sasa kazi ya kuendelea kutoa Elimu ya msingi, Sekondari  na Ufundi iliendelea ikiwa ni pamoja na kuanzisha shule nyingine mpya.

Jumuiya imekuwa wakati wote ikisimamia suala la maadili katika Taifa letu kwa kuzingatia Mila na Desturi za Kitanzania na kuhakikisha kwamba mabadiliko ya Sayansi na Technolojia yanapokelewa kwa tahadhari kubwa bila kuathiri Mila na Desturi.

Kushirikiana na Taasisi za Kiserikali, Binafsi, Mashirika ya Dini kusimamia maadili ya Watanzania, wawepo mashuleni, mitaani, nyumba za ibada, mahali pa kazi kwa kuweka taratibu za kufuatwa na kukumbushana wajibu, utamaduni na miiko yake.

Kwa sasa Jumuiya ina shule takribani 52 zenye Wanafunzi na vyuo viwili, kimoja cha kilimo na mafunzo na kingine cha Ufundi

Msisitizo tupeleke watoto wetu katika shule za wazazi kwani zinafanya vizuri


Ada zetu ni nafuu pia kwani shule zetu lengo lake ni kumsaidia mtoto aliyekosa shule za Serikali na wazazi wake hawana uwezo mkubwa.

Pamoja na kutoa Elimu, Pia imekuwa tanuri la kuwaandaa viongozi wa Nchi yetu ndani ya Chama na Serikali.

Jumuiya hii imekuwa wakati wote mhimili wa CCM katika chaguzi za Serikali za Mitaa na chaguzi za Dola kwa upande wa Tanzania Bara na Tanzania Visiwani.

Jumuiya ya Wazazi imekuwa ikishiriki kikamilifu kufuatilia, kukagua, kushauri na kuelekeza namna bora ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa wakati wote.


Kwa ujumla Jumuiya hii ni moja ya Jumuiya tatu za CCM  zenye malengo na madhumuni ya kuhakikisha zinaitafutia CCM Wanachama na kuhakikisha inashinda uchaguzi wakati wote.

Ndugu Wananchi, mwaka 2019 Jumuiya imetimiza miaka 65 ya kuanzishwa kwake. Sherehe hizi zilizofanyika Kitaifa Mkoani Rukwa aidha sherehe hizi zimefanyika kila Mkoa kwa Nchi nzima.

Pamoja na mambo mengine sherehe hizi zimeadhimishwa kwa kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Hospitali, Vituo vya Afya, Zahanati, Shule za Msingi na Sekondari, Shule ya Watoto wenye ulemavu wa ngozi (Albino) na wasioona, kutembelea watoto waishio katika mazingira magumu, utunzaji wa mazingira, kufanya usafi kwenye maeneo ya utoaji wa huduma za kijamii, michezo mbalimbali, madarasa ya Itikadi za semina elekezi za utendaji kazi ndani ya Jumuiya, Chama na Serikali.

Aidha kufanya Mikutano ya ndani ya kujengeana uwezo  kukagua  miradi  ya maendeleo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya

uchaguzi ya mwaka 2015 – 2020 kuelekea katika kilele cha sherehe hizi Wananchi wamekuwa wakikumbushwa mwaka 2019 ni mwaka wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, na hivyo tunatakiwa kufanya maandalizi mazuri ya kupata Viongozi bora na si bora Viongozi.

Ndugu Wananchi mwaka huu ni mwaka wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kauli mbiu ya Jumuiya kuelekea Uchaguzi ni “ELIMU,  MALEZI  NA MAADILI NI MSINGI WA VIONGOZI   
    CHAGUA VIONGOZI MAKINI 2019”

Kupitia kauli mbiu hii, ituongoze katika kupata Viongozi mwaka huu. Msisitizo unawekwa na kukemea kwa nguvu zote kuundwa kwa makundi ndani ya CCM, tuache Udini, Ukabila au eneo analotoka mtu. Tuwe wamoja kwani mshikamano wetu ndio ushindi wetu.

Ndugu Wananchi, Tumekuwa Mkoani Rukwa tangu tarehe 31/03/2019, Uzinduzi wa sherehe ulifanyika Wilaya ya Nkasi tarehe  01/04/2019 uliofanywa na  Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Ndugu Erasto Sima. Katika siku sita (6) tulizosherehekea  Mkoani   Rukwa  tumeweza  kwenda  Wilaya
zote nne za Kichama ndani ya Mkoa na tumeshiriki shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na miradi katika sekta ya Afya, Elimu, Kilimo, Usafi wa Mazingira na kufanya vikao vya Viongozi na Wanachama na kukumbushana majukumu yetu.

Tunawapeni hongera sana kwa namna mnavyofanya kazi za kusimamia na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi kwa vitendo. Tunawapongeza watendaji wote wa Serikali kwa ngazi zote wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Wenyeviti wa Halmashauri, Wabunge na Madiwani, Watumishi wote wa ngazi mbalimbali kwa namna mnavyofanya kazi kwa bidii.




Aidha tunawapongeza Viongozi wote wa Chama Cha Mapinduzi ngazi zote wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa Ndugu Rainer Lukarah na Wilaya, Chama na Jumuiya zote kwa kuisimamia vyema Serikali yetu.

Tunaipongeza Jumuiya ya Wazazi Mkoa inayoongozwa na Ndugu Enos Budodi kwa kazi kubwa walioifanya katika kuisaidia CCM kutekeleza majukumu yake vizuri.  Mwenyekiti na Viongozi wenzako Hongereni sana.

Tunawapongeza Wanachama kwa ujumla wao namna mnavyounga juhudi za Serikali yetu kwenye shughuli za maendeleo katika kutekeleza Ilani yetu ya Uchaguzi.

Kipekee tunampongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania DR. JOHN POMBE JOSEPH   MAGUFULI   kwa   kazi   kubwa  na  nzuri  anazofanya


kusimamia na kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 – 2020. Rais wetu amefanya na anaendelea kufanya mambo mengi mazuri sana ndani ya kipindi kifupi yakiwa ni pamoja na usimamizi imara na makini wa Serikali, Ulinzi na Usalama, Ujenzi wa miradi mipya ya barabara, Madaraja, Viwanja vya ndege, Ununuzi wa ndege mpya, Miradi mikubwa ya umeme, Ujenzi wa Hospitali mpya, Vituo vya Afya, Zahanati, Utoaji wa Elimu bure, kufufua na kujenga viwanda vipya, ukarabati wa Reli na ujenzi wa Reli mpya ya kisasa (SGR). Hii ni kutaja kwa uchache.

Tunampa hongera sana yeye na Wasaidizi wake wote wakiwepo Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Ndugu Kassim Majaliwa. Tunampongeza pia Rais wa Zanzibar na



Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamedi Shein kwa kazi kubwa ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi kwa vitendo.

Ndugu Wananchi pamoja na mambo mazuri yote tuliyoyafanya ndani ya Mkoa wetu pia zipo changamoto ndogo ndogo zilizopo kwa baadhi ya maeneo  mfano upungufu wa Waalimu, upungufu wa maabara, upungufu wa Zahanati na upungufu wa Watumishi wa Idara ya Afya, changamoto ya bei ndogo za mazao na hasa mahindi, miundombinu ya barabara za vijiji n.k, yote hii tunatoa maagizo kwa uongozi wa Mkoa na Serikali kushughulika nazo pamoja na nyingine nyingi.

Ndugu Wananchi pamoja na kufanya shughuli za maendeleo hatukusahau kufanya kazi za kuimarisha Chama na Jumuiya tumehimiza na kusisitiza suala la Uhai wa Chama na Jumuiya kwa kuhakikisha Viongozi wanazingatia Katiba na Kanuni zetu. Tumehimiza ufanyikaji wa vikao, ziara, semina, kuingiza Wanachama wapya, kulipia Ada za Uanachama na kushiriki katika shughuli za maendeleo na kuisemea CCM kila wakati.

Tunaagiza Mikoa yote Bara na Visiwani kuhakikisha suala la Uhai wa Chama linatiliwa kipaumbele kwa ngazi zote kuanzia ngazi ya
Shina, Tawi, Kata, Jimbo, Wilaya, Mkoa hadi Taifa. Imetolewa Rai kwa CCM kuacha makundi ndani ya Chama na hasa kipindi hiki cha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.  Tudumishe Amani na Mshikamano.

Mwisho nimalizie kwa kutoa tena pongezi nyingi kwa Uongozi wote wa Mkoa Chama, Jumuiya na Serikali kwa maandalizi mazuri na yaliyofanikisha sherehe hizi za wiki ya Wazazi Kitaifa.  Hongereni sana Tunasisitiza yale yote tuliyoagiza na kuyaelekeza basi yaweze kufanyiwa kazi, mkitambua kuwa ndio wajibu wenu katika Mkoa wetu.  Viongozi wa Chama na Jumuiya Mkoa hakikisheni mnafanya ufuatiliaji na kutoa taarifa Makao Makuu.





Nimalizie kwa kumshukuru Mungu kwa kutuongoza vema wiki nzima na  tunamuomba atusimamie pia tunaporudi maeneo yetu.
Naomba sasa kuchukua nafasi hii kutangaza rasmi sherehe za Wiki ya Wazazi Kitaifa zimefungwa rasmi.

AMINA!!




 “KIDUMU    CHAMA     CHA    MAPINDUZI”



UCHUNGU WA MWANA

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages