Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina Michael Lynk amesema upokonyaji wa raslimali za Wapalestina unaofanywa na utawala haramu wa Israel katika maeneo ya Palestina ni uporaji wa wazi.
Akizungumza Jumatatu mjini Geneva, alipowasilisha ripoti yake kwa baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa Bwana Lynk alisema, takribani Wapalestina milioni 5 wanaoishi katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu wameshuhudia namna utawala wa Israel unavyoharibu vyanzo vyao vya maji, kuwapokonya maliasili zao na kuharibu mazingira yao na hivyo kuvuruga maisha yao ya kila siku.”
Ripoti ya Lynk imejikita katika katika masuala yamazingira na maliasili katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel. Ripoti hiyo imesisitiza kuwa watu wanaoishi katika eneo linalokaliwa wanastahili kufurahia haki za binadamu kikamilifu kama zinavyotamkwa katika sheria za kimataifa ili kulinda umoja wao juu ya utajiri wao wa asili.
Mtaalamu huyo amesema utajiri wa asili na madini katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaporwa na Israel kwa manuafaa yao wakati Wapalestina wanayimwa haki zao.
Aidha amesema kuna malalamiko kuwa utawala wa Israel umekuwa ukimwaga taka zenye sumu katika maeneo ya Ukingo wa Magharibi.
Ripoti pia imezungumzia kuhusu namna utawala wa Kizayuni wa Israel unavyotumia mabavu dhidi ya waandamanaji Wapalestina. Pia bwana Lynk ameeleza hofu yake kuhusu mustakabali wa familia takribani 200 za Wapalestina walioko Quds (Jerusalem) Mashariki ambao wako katika hatari ya kufurushwa kutoka katika ardhi zao za jadi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇