Serikali ya Pakistan imetangaza kwamba itamrejesha balozi wake Sohail Mahmood, nchini India baada ya kumwita nyumbani kufuatia mgogoro wa hivi karibuni kati ya nchi mbili. Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan imemwita mwambata wa ubalozi wa India mjini Islamabad na kumtaarifu habari ya kurejea mjini New Delhi, balozi wake huyo.
Itakumbukwa kuwa baada ya kushtadi mzozo kati ya Pakistan na India, nchi hizo ziliwaita nyumbani mabalozi wao. Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan, Shehryar Khan Afridi amesema kuwa, mapambano dhidi ya makundi yaliyopigwa marufuku nchini humo, ni uamuzi uliochukuliwa kitambo na serikali ya Islamabad. Afridi ameyasema hayo leo katika kikao na waandishi wa habari na kusisitiza kwamba Pakistan iko mbioni kuyaangamiza makundi ya wabeba silaha yaliyopigwa marufuku na yale ya kigaidi sambamba na kuyafungia akaunti zao za fedha. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan ameongeza kwamba, operesheni dhidi ya makundi ya kigaidi hazitakomea kwa makundi fulani.
Bendera za India na Pakistan
Naye kwa upande wake Wizara ya Vyombo vya Habari ya nchi hiyo imesema kuwa, hatua dhidi ya makundi ya kigaidi, ni uamuzi uliochukuliwa tangu mwezi Januari mwaka huu na ambao sasa umeingia katika hatua za kiutendaji. Hii ni katika hali ambayo kwa muda sasa serikali ya India imekuwa ikiilaumu Pakistan kwa kushindwa kuchukua hatua kali dhidi ya makundi ya kigaidi yanayotekeleza jinai na uhalifu ndani ya ardhi ya India. Duru mpya ya mgogoro kati ya nchi hizo iliibuka baada ya kundi la kigaidi linalojiita Jaish-e-Mohammed kufanya shambulizi katika eneo la Kashmir lililo chini ya udhibiti wa India tarehe 14 mwezi jana na kupelekea kwa akali watu 44 kuuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa. Wiki moja baada ya shambulizi hilo, ndege za kivita za India zilifanya mashambulizi makali katika ngome za makundi ya kigaidi ndani ya ardhi ya Pakistan ambapo watu 300 waliripotiwa kuuawa, huku Islamabad nayo ikilipiza kisasi.
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇