Serikali itaendelea kusimamia na kudhibiti matumizi ya kemikali ili kuhakikisha hazileti madhara kwa afya za wananchi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu leo alipokuwa kwenye mkutano na wadau wa kemikali kujadili namna ya kuboresha mazingira ya kufanya biashara ya kemikali nchini.
“Kemikali zisipodhibitiwa vizuri zinaweza kuleta madhara katika afya, mazingira pamoja na kuhatarisha usalama wa nchini, ipo haja ya kuweka mazingira mazuri ya kusimamia na kudhibiti uingizaji na matumizi ya kemikali nchini ili zisilete madhara” amesema Waziri Ummy.
Hata hivyo takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2014 zinaonyesha vifo milioni 12.6 vilitokana na mazingira duni ya kuishi, mojawapo ya kichocheo ni athari za kemikali ambazo zimekuwa zikisababisha magonjwa na vifo.
Waziri Ummy amesema kuwa kemikali zimekuwa na athari kubwa kwa binadamu kwa kusababisha magonjwa zaidi ya 100 huku akiyataja magonjwa ya moyo, saratani, ngozi, athari katika mifumo ya fahamu, upumaji pamoja na chakula kuathiri zaidi wananchi wengi.
“Tukubali kuwa kemikali zina madhara kwa wananchi lakini sasa tuwe na mazingira mazuri ya kuzidhibiti” amesema Waziri Ummy na kuendelea kusema kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira mazuri kwa wafanya biashara ya kemikali nchini.
Kwa upande mwingine Waziri Ummy amezitaka Taasisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) pamoja na Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) kuangalia upya tozo wanazotoza kwa wafanyabiashara za kemikali nchini pamoja na kupunguza urasimu usiokuwa na ulazima ili kuwawekea mazingira rafiki wafanya biashara za kemikali.
“Msiwe ni kikwazo kwa uwekezaji na biashara, kikwazo cha kushamiri na kukua kwa uwekezaji nchini, nataka muwe mawakala wa kukuza biashara na uchumi nchini” amesema Waziri Ummy.
Awali akisoma taarifa yake Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko amesema Sheria ya Kemikali ya mwaka 2003 imekuwa na mchango mkubwa katika udhibiti wa matumizi ya kemikali nchini.
“Kabla ya kutungwa kwa sheria hii, kemikali zilikuwa zikiingizwa nchini kiholela na kutumika bila ya kuwa na ufatiliaji au udhibiti wowote” alisema Dkt. Mafumiko.
Dkt. Mafumiko amesema Sheria ya kemikali imewawezesha kudhibiti usafirishaji, utumiaji pamoja uteketezaji wa taka zinazotokana na kemikali.
“Ofisi ya Mkemia inasimamia kwa ukaribu matumizi ya kemikali zote zinazoingizwa nchini kuanzia zinapoingia, mahali zinapokwenda pamoja na matumizi yaliyokusudiwa” alisema Dkt. Mafumiko.
Naye Katibu Mkuu wa Mawakala wa Forodha Tanzania Mhandisi Anthony Swai amesema tozo zimekuwa nyingi kiasi cha kuwaumiza wafanyabiashara wa kemikali huku urasimu pia ukisababisha wafanyabiashara kutumia muda mwingi kufuatilia vibali vya uingiza wa kemikali nchini.
Aidha Mhandisi Swai ameiomba Serikali kuainisha mipaka ya taasisi za umma pamoja na tozo wanatostahili kulipa kwani kumekuwa na mwingiliano wa majumuku baina ya taasisi za Serikali ambazo amezijata kuwa ni GCLA, TDFA na TBS (Shirika la Viwango Tanzania)
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇