Idadi ya watu waliouawa kutoka jamii ya Fulani katika mapigano ya hivi karibuni katika nchi ya Mali iliyoko magharibi mwa Afrika imeongezeka na kufikia 157.
Hayo yameelezwa na msemaji wa serikali ya Mali huku akibaini kwamba, machafuko hayo ni mabaya katika historia ya hivi karibuni ya nchi hiyo. Awali serikali ilikuwa iimetangaza kwamba watu 135 kutoka jamii ya Fulani waliuawa katika mashambulio hayo.
Mauaji hayo yametokea katika kipindi kilicho chini ya wiki moja baada ya kutokea shambulizi la kigaidi dhidi ya kambi moja ya kijeshi lililosababisha jumla ya askari 23 kuuawa.
Kundi moja la kigaidi na ukufurishaji lenye mahusiano na genge la al-Qaidah lilitangaza kuhusika na shambulizi hilo. Raia wa Mali wamekuwa wakilalamikia udhaifu wa jeshi la nchi hiyo na wamelitaka lidhibiti vitendo vya jinai na mauaji na pia kuwalinda.
Kufuatia kushtadi vitendo vya ukatili nchini Mali na pia kuuawa makumi ya watu wa jamii ya Fulani na wabeba silaha, Rais Ibrahim Boubacar KeĂŻta wa nchi hiyo alitangaza kumpiga kalamu nyekundu mkuu wa majeshi na kamanda wa kikosi cha ardhini katika nchi hiyo.
Licha ya askari 4500 wa Kifarasa kuwepo katika eneo la Sahel mwa Afrika, lakini mashambulizi ya kigaidi yameshika kasi katika eneo hilo. Askari hao wa kigeni walifika eneo hilo mwaka 2013 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇