Muungano wa Madaktari nchini Sudan umesema, watu 57 wameuawa hadi sasa tangu yalipoanza maandamano ya kupinga serikali tarehe 19 Disemba mwaka jana.
Taarifa ya muungano huo imesema madaktari 28 wamekamatwa kufikia sasa kwa kushiriki maandamano hayo, na kwamba mmoja wa madaktari hao aliuawa kwa kupigwa risasi na maafisa usalama akiwa katika maandamano hayo.
Kadhalika taarifa ya Muungano wa Madaktari nchini Sudan imelaani hatua ya vyombo vya usalama kuendelea kutumia nguvu kupindukia kukabiliana na waandamanaji hao.
Hii ni katika hali ambayo, serikali ya Khartoum inadai kuwa waliouawa hadi sasa katika maandamano hayo hawafiki watu 30.
Taarifa hiyo ya muungano wa madaktari imetolewa siku moja baada ya Idara ya Upelelezi kusema kuwa mmoja wa shakhsia wa kisiasa wanaoongoza maandamano hayo kwa jina Ahmed al-Khair alipoteza maisha akiwa kizuizini baada ya kupigwa na maafisa usalama.
Maandamano nchini Sudan awali yalichochewa na hatua ya serikali ya kupandisha mara tatu bei ya mkate; lakini sasa yamegeuka na kuwa maandamano dhidi ya utawala wa miongo mitatu wa Rais Omar al-Bashir.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇