Wadau wa madini na wachimbaji wa mkoa wa Manyara, wanatarajia kuandamana Jumamosi ijayo, kwa lengo la kumshukuru Rais John Magufuli kwa kukubali kutia saini muswaada wa dharura wa marekebisho ya sheria za fedha, kupunguza na kufuta kodi zilizolalamikiwa.
Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Manyara
(Marema), Tawi la Mirerani, Shwaibu Mushi, alisema jana kuwa
maandalizi ya maandamano hayo yatakayopokelewa na Mkuu wa Mkoa huo,
Alexander Mnyeti, yanaendelea vizuri.
Alisema maandamano yatafanyika umbali wa kilomita tatu na yataanzia
kwenye lango la Magufuli la kuingia ndani ya ukuta saa 2:00 asubuhi
na kumalizika Saa 4:00 asubuhi.
Baada ya hapo, alisema itasomwa risala ya kumpongeza
Rais Magufuli kudhibiti utoroshwaji madini, ulipaji kodi na kumuunga
mkono.
“Waandamanaji watazunguka migodi ya madini ya Tanzanite hadi kwenye
uwanja wa barafu wa CCM Mji Mdogo wa Mirerani ndipo
watakapoishia,”alisema.
Mushi alisema maandamano hayo yatawahusisha wachimbaji wote wa madini
wa mkoa huo kutoka wilaya zote za Simanjiro, Kiteto, Babati, Hanang'
na Mbulu.
Alisema lengo kubwa ni kumpongeza Rais Magufuli kwa kuwakubalia
ombi lao, hadi wabunge wakapitisha sheria hiyo baada ya mkutano wa
kisekta wa wadau wa madini uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es
Salaam.
Alisema kaulimbiu ya maandamano hayo ni “Rais Wetu, Madini Yetu,
Uchumi Wetu” na wadau mbalimbali wa madini wakiwamo wachimbaji,
wamiliki wa migodi na wazamiaji (na Apolo) watashiriki.
"Pia wadau wengine wanaonufaika na madini wakiwamo wafanyabiashara,
madalali na wanunuzi wa madini, watashiriki maandamano hayo
ya kumpongeza Rais Magufuli wetu," alisema Mushi.
Alisema wanaandamana kumpongeza Rais Magufuli, baada ya kupita siku 17
tangu mkutano wake na wadau wa madini kufanyika na kisha kupitishwa
kuwa sheria na bunge.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Agustino Senga
alisema maandamano kama hayo yanaruhusiwa kufanyika mradi
wahusika wawe na kibali kutoka kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya husika.
Kamanda Senga alisema hivi karibuni yalifanyika maandamano kama hayo
ya wafugaji na wakulima kumpongeza Rais Magufuli kwa kuwatetea, hivyo
hata hayo ya wadau wa madini watayaruhusu wakiomba kibali.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇