Sambamba na kuendelea mgogoro wa kisiasa nchini Venezuela, wapinzani wa serikali wanaoungwa mkono na Marekani wamezidisha njama zao za kubadilisha hali ya nchi hiyo kwa anufaa yao.
Hivi sasa serikali ya Marekani inatumia nyenzo za kiuchumi dhidi ya serikali ya mrengo wa kulia ya Rais Nicolás Maduro wa Venezuela na wakati huo huo inatishia kutumia nguvu ya kijeshi kumuondoa madarakani rais huyo aliyechaguliwa kikatiba na wananchi. Hii ni katika hali ambayo wapinzani wa nchi hiyo ya Amerika ya Latini wanataka kutumia uvamizi wa kijeshi wa madola ya kibeberu kumuondoa madarakani raia huyo. Ijumaa iliyopita, Juan Guaidó kiongozi wa upinzani hakukanusha kuweko uwezekano wa uingiliaji kijeshi wa Marekani dhidi ya serikali ya Caracas na kuongeza kwamba, iwapo italazimu yuko tayari kuisaidia na kuungana na Marekani katika njama za kuingilia kijeshi na kumuondoa madarakani kwa nguvu Rais Maduro. Kadhalika Guaidó alidai kwamba lengo la hatua hiyo ni kuhitimisha mgogoro unaoendelea nchini Venezuela. Itakumbukwa kuwa mgogoro mpya wa kisiasa nchini Venezuela ulizuka tarehe 23 Januari mwaka huu baada ya Juan Guaidó, kiongozi wa upinzani anayeungwa mkono na madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani kujitangaza kuwa rais wa muda wa nchi hiyo, hatua ambayo ilitajwa na serikali ya Caracas kuwa ni mapinduzi dhidi ya Rais Nicolás Maduro aliyechaguliwa na wananchi.
Hivi karibuni pia rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza kwamba, anafikiria kuivamia kijeshi Venezuela kama njia ya kupambana na Rais Nicolas Maduro. Hii ni katika hali ambayo akthari ya nchi za dunia, ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia, China, Cuba, Uturuki, Afrika Kusini, Uruguay, Italia, Korea Kaskazini na kadhalika, zimelaani vikali hatua hiyo ya Marekani na washirika wake kama ambavyo zimesisitizia umuhimu wa kuheshimiwa haki ya kujitawala ardhi yote ya Venezuela.
Kuna dalili za kila namna zinaonyesha uwezekano wa kutekelezwa tishio la Marekani la kuivamia kijeshi Venezuela kwa ajili tu ya kumuingiza madarakani kibaraka wake Juan Guaidó. Baadhi ya duru za habari zimearifu kuwa, kibaraka huyo wa nchi za Magharibi amefanya mawasiliano ya simu ya moja kwa moja na ikulu ya Marekani White House na baadhi ya askari wa Venezuela kwa ajili ya kuwatisha na kuwarubuni ili wafanye mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali ya Caracas. Kiongozi mmoja wa ngazi ya juu ambaye hakutaka kutaja jina lake amefichua kwamba hivi sasa Marekani inajiandaa kuanzisha duru mpya ya vikwazo dhidi ya Caracas na wakati huo huo imefanya mawasiliano ya moja kwa moja na askari wa Venezuela. Afisa huyo wa Marekani ameendelea kusema kuwa, Washington imewataka askari hao waache kumuunga mkono Rais Nicolás Maduro na badala yake wamuunge mkono Juan Guaidó, kibaraka wa madola ya kibeberu ya Magharibi.
Hata hivyo na licha ya njama kubwa za Marekani katika kuwarubuni makamanda wa ngazi ya juu wa jeshi la Venezuela, hadi sasa ni idadi ndogo sana ya askari wa nchi hiyo waliomsaliti Rais Nicolás Maduro. Ni kwa ajili hiyo ndio maana viongozi wa Marekani wamekiri kwamba hadi sasa Washington haijaamini kwamba mawasiliano ya simu iliyoyafanya yataweza kuibuka mpasuko katika safu ya waungaji mkono wa Rais Maduro au la. Hasa kwa kuzingatia kuwa, kabla ya hapo pia Marekani na wapinzani wa serikali ya Venezuela waliwashawishi askari hao ingawa hata hivyo hawakupata mafanikio yoyote na badala yake jeshi la Venezuela limeendelea kuwa pamoja na rais huyo aliyechaguliwa na wananchi. Marekani na washirika wake sambamba na kuiwekea vikwazo na kuwaunga mkono kwa hali na mali wapinzani wa Venezuela, inafanya pia njama za kuiondoa madarakani serikali halali ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa Rais Nicolás Maduro, Washington inafanya njama ya kuitumbukiza Venezuela katika ghasia na machafuko ingawa amesisitiza kwamba kamwe haitofanikiwa. Marekani inayojiona kuwa ni yenye nguvu duniani inadhani kwamba kwa kutumia mabavu na udikteta, inaweza kuzitwisha nchi nyingine matakwa yake. Hata hivyo mataifa mengine yenye nguvu kama vile Russia, China na nchi nyingine wapinzani wa ubeberu wa Washington katika maeneo tofauti ya ulimwengu, yanapinga vikali ubeberu huo wa Marekani. HIvi sasa dunia imeingia katika makabiliano makali kuhusiana na mustakbali wa Venezuela. Katika makabiliano hayo, kambi ya Magharibi ikiongozwa na Marekani na washirika wake katika eneo la Amerika ya Latini, inataka kuiondoka madarakani serikali halali ya Rais Nicolás Maduro licha ya kwamba wananchi wanamtaka rais huyo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇