Rais wa Marekani Donald Trump jana Ijumaa alitangaza hali ya dharura ya kitaifa, hatua ambayo inampa uwezo wa kuhamisha fedha kutoka sehemu nyingine katika bajeti ya serikali kuu na kuzitumia kwa ujenzi wa ukuta kati ya Marekani na Mexico, ambao umezua utata.
Trump, alisema hatua ya kutangaza hali ya dharura inalenga kuangamiza ulanguzi wa dawa za kulevya, uhalifu na makundi ya uhalifu anaodai wanaingia Marekani kupitia mpaka wa kusini.
Hatua ya Trump inajiri baada ya baraza la waakilishi na Seneti kukataa kumpa dola bilioni 5.7 kwa ajili ya ujenzi wa ukuta huo.
Mswada wa Seneti, unampa dola bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa takriban kilomita 90 ikiwa ni chini ya kiwango cha awali alichotaka cha dola bilioni 5.7 kwa ujenzi wa ukuta wenye urefu wa kilomita 322.
Trump hata hivyo alisema kufuatia hatua yake ya kutangaza Dharura ya Kitaifa, anatarajia upinzani mkubwa mahakamani lakini akasema yupo tayari kuitetea kutoka mahakama ya chini hadi ya juu akieleza imani kwamba mwishowe, atapata pesa anazotaka kwa ujenzi wa ukuta huo.
"Ninajua nitapelekwa mahakamani, lakini niko tayari kutetea hatua yangu hadi kwa mahakama kuu," alisema Trump.
Lakini muda mfupi baada ya rais huyo kutoa kauli hiyo, Spika wa baraza la wawakilishi la Marekani, Nancy Pelosi na kiongozi wa walio wachache kwenye Seneti, Chuck Schumer, wametoa taarifa ya pamoja na kusema kwamba hawatamruhusu rais Trump 'kuikatakata vipandvipande" katiba ya Marekani.
Sera ya uhamiaji kwa jumla, hususan suala la ujenzi wa ukuta, limezua mgawanyikao mkubwa kisiasa Marekani, na lilipelekea kufungwa kwa baadhi ya shughuli za serikali kwa siku 35, hatua ambayo ilikosolewa vikali na wapinzani wa Rais Trump.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇