LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 24, 2019

MGOMO WA CHAKULA MASHEIKH KATIKA JELA YA SAUDI ARABIA

  • Sambamba na Sheikh Abdullah Hamid Ali al-Hamid, kiongozi wa kidini na mwanaharakati wa sheria nchini Saudi Arabia kususia kula chakula katika moja ya jela za nchi hiyo, wafungwa wengine wanaozuliwa katika korokoro za utawala wa Aal-Saud nao pia walianzisha mgomo huo.
Zaidi ya wafungwa elfu 30 wa kisiasa wanazuiliwa katika jela za kutisha za utawala wa Saudi Arabia. Makosa ya wafungwa hao nchini humo yanatajwa na serikali kuwa makosa makubwa, na hii ni kwa kuwa mafungwa hao ni wakosoaji wa siasa za utawala wa Aal Saud. Hasa kwa kuzingatia kuwa utawala huo si tu kwamba haukubali kukosolewa, bali ni kwamba kwa mujibu wa mafundisho ya Uwahabi, kitendo cha kukosoa serikali, kinahesabika kuwa ni kosa kubwa. Miongoni mwa wafungwa wa kisiasa wanaozuiliwa katika jela za Aal-Saud ni pamoja na mawakili wakubwa, majaji, wasomi wa vyuo vikuu, watafiti wa Kiislamu, wanaharakati wa vyombo vya habari, maulama na mubalighina wa kidini. Mfumo wa mahakama nchini Saudi Arabia nao hauna uadilifu, na hii ni kwa kuwa wafungwa hao bila ya kuelezwa tuhuma zao, huwa wanahukumiwa tu vifungo vya muda mrefu vya kuanzia miaka 10 na kuendelea. Mbali na hayo, wafungwa hao wanafanyiwa vitendo vibaya kiasi kwamba utawala wa Aal-Saudi hauzingatii hata kidogo suala la kuendelea maradhi ya kuambukiza kati ya wafungwa.


Hukumu za kidhalimu zinazotolewa ovyo dhidi ya wafungwa ambao hata huwa hawajashtakiwa

Hali ni mbaya zaidi kwa wafungwa wa kidini na kisiasa, na hii ni kwa kuwa utawala wa Aal-Saud unaitakidi kwamba wafungwa hao wa kidini si wakosoaji wa masuala tu ya kisiasa, bali ni wakosoaji pia wa fikra za madhehebu yanayotawala nchini Saudia ambayo ni ya Uwahabi. Ili kuwahukumu kwa vifungo vizito wafungwa hao wa kisiasa na kidini, utawala wa Saudia kwanza huwa unawatuhumu kwa makosa bandia kama vile ya kufanya ujasusi kwa ajili ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mwezi Septemba mwaka jana mtandao wa habari wa The Middle East Monitor uliripoti kwamba, watawala wa Saudia waliwatia mbaroni makumi ya vijana kwa madai bandia ya kukusanya silaha na kuwa na uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ama suala jingine ni kwamba, baada ya kuteuliwa Mohammad Bin Salman kuwa Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia, idadi ya wafungwa wa kisiasa, vitendo vibya dhidi ya wafungwa na kutolewa hukumu zisizo za kiadilifu, vimeongezeka sana nchini humo. Hadi sasa mashirika ya kimataifa kama vile Shirika la Kutetea Haki za Binaadamu la Human Rights Watch na Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International, yametaka kuachiliwa huru haraka wafungwa hao na angalau kupunguzwa vitendo vya ukatili dhidi yao. Idris Saleh, mjumbe wa Ofisi ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa, sambamba na kubainisha kwamba utawala wa Mfalme Salman bin Abdulaziz Aal Saud na Mohammad Bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia unakandamiza sana misingi ya haki za binaadamu, alisema kuwa, ofisi ya kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa amewataka watawala wa nchi hiyo kuwaachilia huru haraka iwezekanavyo mamia ya wanaharakati ya kisiasa na kisheria ambao wamewekwa kizuizini kwa sababu tu ya kubainisha mitazamo yao.


Ukoo wa kidikteta wa Aal-Saud ambao unafanya ukandamizaji dhidi ya wapinzani na wakosoaji wake

Kadhalika kuongezeka idadi ya wafungwa wa kisiasa na pia mgomo wa kususia chakula kunakofanywa na mubalighina wa kidini kunaakisi ukweli huu kwamba, Mfalme Salman na mwanawe Mohammad Bin Salman hawazingatii hata kidogo matakwa na ukosoaji wa kimataifa dhidi yao. Ukweli ni kwamba, kadri ukosoaji wa asasi za kimataifa unavyoongezeka katika kulaani ukandamizaji wa kutisha wa kisiasa na vyombo vya mahakama vya Saudia, ndivyo utawala wa Aal-Saud unavyozidi kushadidisha ukatili nchini humo. Aidha suala jingine muhimu ni kwamba, mgomo wa kususia chakula wa mubalighina wa kidini katika jela za utawala wa Aal-Saud, unaungwa mkono na raia wa nchi hiyo. Raia wa Saudia ambao hawana haki ya kufanya maandamano na ambao wanatambua kwamba ukosoaji wowote wa maneno dhidi ya serikali huwa unakabiliwa na adhabu kali, wameanzisha kampeni katika mitandao ya kijamii ya kuwaunga mkono wafungwa wa kisiasa wakiwemo pia viongozi wa kidini wanaoshikiliwa katika jela. Baada ya kuanzishwa na wasomi wa kidini mgomo wa kususia chakula, mitandao ya kijamii nchini Saudia imeshuhudia wimbi kubwa la kampeni iliyopewa jina la 'Mgomo wa Masheikh katika Jela za Aal-Saud.' Ama nukta ya mwisho ni kwamba, licha ya baadhi ya viongozi wa nchi za Magharibi kupitia vyombo vya habari kulaani vikali jinai na mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari mkosoaji wa utawala wa Aal-Saud, sambamba na kukosoa utawala wa nchi hiyo kiasi cha kufikia kusisitizia udharura wa kusitishwa uuzaji silaha kwa Saudi Arabia, lakini pamoja na hayo hawako tayari kuwaunga mkono wafungwa wa kisiasa na kidini wanaoteseka katika jela za Saudi Arabia.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages