Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Iran amesema maadui wa Jamhuri ya Kiislamu wameshadidisha jitihada zao za kueneza chuki dhidi Iran (Iranophobia) wakiwa na tamaa na lengo la kusaini mauzo ya silaha zao na nchi za eneo la Mashariki ya Kati.
Meja Jenerali Muhammad Hossein Baqeri alisema hayo jana hapa mjini Tehran katika kikao na waandishi wa habari na kuongeza kuwa, katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, Jamhuri ya Kiislamu haijawahi kuwa na tamaa ya kupora milki ya nchi yoyote ile katika eneo hili, lakini imekuwa tu na washauri katika baadhi ya nchi za eneo tena kwa mwaliko wa nchi husika zinazopambana na kero la ugaidi.
Amefafanua kwa kusema, "Iran imetuma washauri wake katika nchi za Syria na Iraq kwa ombi la serikali za nchi hizo zinazopambana na magaidi wa kitakfiri, na uwepo wetu katika nchi hizo utasalia kama ulivyo, iwapo serikali hizo zitaendelea kutuhitaji. Hii ni kinyume kabisa na Marekani ambayo imezivamia nchi za eneo bila riadhaa ya wananchi na serikali, huku ikiituhumu Iran kuwa inaingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine."
Kwengineko katika mazungumzo yake hayo ya jana, Meja Jenerali Muhammad Hossein Baqeri ameashiria matamshi ya hivi karibuni ya Umoja wa Ulaya kuhusu uwezo wa makombora na kujihami Iran na kubainisha kuwa, makelele ya maadui na vitisho vyao katu havitaishurutisha Iran ifanye mazungumzo kuhusu uwezo wake wa makombora.
Ameongeza kuwa, badala ya nchi za EU kujishughulisha na uwezo wa kujihami Iran, zingelipaswa kuwa mbioni kuondoa vizingiti katika miamala ya kibenki na kibiashara kati yao na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kama sehemu ndogo ya kuonesha kufungamana kwao na makubaliano ya nyuklia ya Iran yanayofahamika kama JCPOA.
Amesisitiza kuwa, wataalamu wa kijeshi wa Iran wana uwezo wa hali ya juu katika kukidhi mahitaji ya kiulinzi ya taifa hili.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇