-------
Na Mwandishi Maalum, Bukoba
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wahakikishe wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia katiba ya chama ili kuepusha migogoro kwenye maeneo yao.
Amesema chama chochote ambacho viongozi wake hawazingatii katiba lazima kiwe na migogoro kwani uzingatiaji wa katiba ni miongoni mwa mambo yanayokitofautisha Chama Cha Mapinduzi na vyama vingine vya siasa nchini.
Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Februari 21, 2019) wakati akizungumza na viongozi wa CCM, wabunge pamoja na baadhi ya viongozi wa mkoa wa Kagera kwenye Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera kilichofanyika katika ukumbi wa ELCT.
Waziri Mkuu ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Mlezi wa CCM mkoa wa Kagera amesema ni muhimu kwa viongozi hao kusoma na kuizingatia katiba ya chama kwa sababu inaelekeza misingi yote ya utendaji.
Amewasisitiza wanachama na wapenzi wa CCM wasome katiba ya chama na kuzielewa kanuni, taratibu na sera ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Akisisitiza jambo hilo Waziri Mkuu amegawa nakala za katiba ya hiyo kwa viongozi hao na kuwataka wazifikishe hadi kwenye ngazi ya mashina.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa nchi nzima unaendelea vizuri na kuhusu changamoto zilizopo katika baadhi ya maeneo nchini wanaendelea kuzirekebisha.
Amesema lengo lao ni kuhakikisha wanatekeleza ilani kama CCM ilivyoelekeza na ili kujiridhisha kama wanafanya vizuri lazima viongozi wawasimamie watendaji katika maeneo yao na watakapobaini kasoro wasisite kutoa taarifa.
Waziri Mkuu amesema viongozi chama lazima wajiridhishe kama huduma za maji, elimu, miundombinu ya barabara, kilimo pamoja nishati ya umeme zinapatikana kwenye maeneo yao yote na ni kwa kiasi gani.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇