Jeshi la Polisi mkoani Dodoma, linamshikilia mkazi wa Chikoa, William Saimon (28), kwa tuhuma za kumkaba na kumbaka bibi kizee Jema Macheho (77), ambaye alifariki dunia baadaye wakati akipatiwa matibabu.
Hayo yalielezwa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa.
Muroto alisema mtuhumiwa huyo alimkaba na kumbaka bibi kizee huyo ambaye ni mkazi wa Bihawana ambaye alifariki dunia katika Hospitali ya Rufani ya Dodoma akiwa anapatiwa huduma ya kwanza.
Alisema tukio hilo lilitokea Jumatatu saa 5:55 usiku katika kijiji cha Bihawana wakati marehemu akiwa njiani kurudi nyumbani kwake.
"Akiwa njiani ghafla alikutana na mtuhumiwa na kumvutia vichakani kwa kumkaba shingo na kumfanyia kitendo cha ubakaji,” alisema.
Kamanda Muroto alisema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani kwa kosa la mauaji.
Katika tukio jingine, Muroto alisema jeshi hilo linamshikilia Leusi Lazaro (23), mkazi wa mkoani Dar es Salaam, kwa kudaiwa kuwaibia wanafunzi mali mbalimbali kwenye mabweni ya vyuo vikuu jijini hapa.
Alisema katika Chuo cha Biashara (CBE), mtuhumiwa aliiba kompyuta mpakato (laptop) aina ya Dell Spiral Min ,Chuo cha St. John aliiba simu aina ya Iphone 6+ na Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), aliiba simu mbili aina ya Tekno W2 na Tekno K7.
Alisema mbinu anazotumia ni kuwavizia wanafunzi wa vyuo hivyo wanapoingia madarasani na yeye anaingia kwenye mabweni na kuiba mali zao.
Alitoa wito kwa wananchi walioibiwa Tv aina ya Flat Screen, Lap top, ving’amuzi na simu kufika Kituo Kikuu cha Kati cha Polisi kuzitambua mali zao wakiwa na risiti walizonunulia.
Alisema mali hizo zilikamatwa na jeshi hilo katika msako uliofanyika maeneo mbalimbali ya mkoa huu kuanzia Januari hadi Februari, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇